Monday, March 5, 2018

Jamii imetakiwa kutunza miundo mbinu ya maji inayotengenezwa kwa gharama kubwa


Na. Elinipa Lupembe.

Jamii imetakiwa kushiriki kwa hali na mali kutunza rasilimali maji pamoja na kusimamia miundo mbinu ya maji inayojengwa kwenye maeneo yao kwa kuwa inajengwa kwa gharama kubwa zaidi  ili miradi ya maji inayojengwa iwe endelevu kwa miaka mingi ijayo.    

         Rai hiyo imetolewa na mkuu wa Idara ya huduma za Jamii Idara ya Maendeleo ya Kimataifa  Uingereza 'DFID', Bi. Getrude Mapunda alipokutana na viongozi wa jamii kutoka eneo linalotekelezwa mradi wa maji wa vijiji vitano ndani ya halmashauri ya Arusha maarufu kama mradi wa maji wa WaterAid unaofadhiliwa na Idara ya Maendeleo ya nchini Uingereza 'DFID' kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5.     

      Mapunda amekutana na viongozi hao ili kuthibitisha ushirikishwaji wa jamii katika utekelezaji wa mradi huo ambao tayari miundo mbinu yake imeanza kuchimbwa na unategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa 2018.   

         Licha ya kuridhishwa na uelewa wa pamoja waliokuwa nao viongozi hao baada ya kujengewa uwezo  juu ya mradi huo wa maji, Mapunda amewataka viongozi hao kuendelea kuweka mikakati thabiti ya utunzaji wa mazingira ambayo ndio chanzo kikuu cha upatikanaji wa rasilimali maji.        
   
        Aidha amendelea kufafanua kuwa miradi ya maji inatumia gharama kubwa kujengwa hivyo jukumu kubwa la wananchi ni kuwa na mikakati thabiti ya kuitunza na kuiendeleza miradi hiyo ili iweze kutumika kwa miaka mingi ijayo na vizazi vijavyo.   

      "Ili mradi wa mji uwe endelevu ni jukumu la jamii kutunza  miundo mbinu ya maji ikiwemo kuchangi gharama za maji kwa ajili ya maintainance pamoja na kutunza mazingira ya uhifadhi wa maji" amesema Mapunda.     
                               
          Naye mhandisi wa maji mkoa w Arusha Mhandisi Makaidi amethibitisha hali halisi ya kupungua kwa kiasi cha  maji inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi na kusababisha maji kupungua na kupatikana  kwenye kina kirefu kadiri siku zinavyokwenda tofauti na miaka ya nyuma.     
   
   Amefafanua kuwa suala la utunzaji wa mazingira linapaswa kupewa kipaumbele na jamii nzima ili kuepuka madhara makubwa ya ukosefu wa maji yanayoweza kutokea kwa  siku za baadaye. 

    "Tafiti zinaonesha kwa sasa maji yanapatikana urefu 
wa mita 100 mpaka 150 kwenda chini,  kama tusipochukua hatua madhubuti miaka kumi mpaka ishirini ijayo maji hayo yatapatikana kina cha mita 200 mpaka 300 jambo ambalo litaathiri hata miradi hii inayotekelezwa sasa" amesisitiza Mhandisi Makaidi. 
             
    Hata hivyo viongozi wa jamii wa eneo la mradi wamethibitisha kuunga mkono juhudi za serikali za utunzaji wa mazingira, utunzaji wa miundo mbinu ya maji pamoja na uchangiaji wa gharama za huduma za maji ili kuendeleza miradi hiyo ya maji ambayo  serikali na  wafadhili hutumia gharama kubwa kuijenga.  
                     
       Wameongeza kuwa katika maeneo yao kumekuwa na agenda ya kudumu ya utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi za familia na jamii nzima kwa kuhamasisha wananchi kutunza mazingira.     

       Diwani wa kata ya Olkokola mheshimiwa Kalanga Laizer amesema kuwa wananchi wa kata yake wamehamasika kujenga vyoo bora baada ya kuwa na mkakati wa kutoza faini kwa nyumba isiyokuwa na choo  bora na muitikio ni mkubwa kwa sasa.       

    "Kwa sasa wananchi wa kwetu wana vyoo bora licha ya kuwa bado kuna changamoto ya maji katika maeneo hayo lakini tunaamini mradi huu ukikamilika shida itakwisha. Amesema Mheshimiwa Kalanga.

     Mradi huo wa maji unatekelezwa kwenye vijiji vya Olkokola na Lengijave na vitongoji vya Olmotonyi, Ekenywa na Seuri vya Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 kwa ufadhili wa serikali ya Uingereza kupitia Idara ya Maendeleo ya  Kimataifa  'DFID'.

       Wakati huo huo serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeongeza kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya ujenzi wa mradi huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwezesha kutumia chanzo cha maji cha Emutoto kilichopo kwenye msitu ndani ya hifadhi ya mlima Meru licha ya mradi huo kutumia vyanzo hivyo viwili vya kuchimbwa.

        Mradi huo unategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa  2018 na unategemewa kuhudumia takribani watu 50,000 ambao watapata maji ndani ya mita 400 na kutekeleza mpango wa serikali ya awamu ya tano wa kuhakikisha asilimia 90% ya wakazi wa vijiji kupata maji safi na salama ifikapo mwaka 2025.






No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo