Sunday, August 6, 2017

Elias Ole Naigisa awa tena Makamu Mwenyekiti Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni


Mheshimiwa Elias Ole Naigisa Laizer wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA amechaguliwa tena kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka ya  Mji Mdogo Ngaramtoni baada ya kushika nafasi hiyo kwa miaka mitatu  tangu kuanza kwa mamlaka hiyo mwaka 2014.
Mh. Elias Mollel ametetea kiti chake baada ya kupata kura 15 kati ya kura 25 zilizopigwa na kumshinda mpinzani wake Mhe. Rose Enock mwenyekiti viti maalum kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 10.
Uchaguzi huo umefanyika wakati wa Mkutano Maalumu wa mwaka wa Baraza la Mamlaka na kufanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo ambapo kisheria huchaguliwa kila baada ya mwaka mmoja.
Mtendaji Mkuu Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni ndugu Sophia Shoko amemtangaza Mh. Elias Olenaigisa Mollel ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Namayani kata ya Kiranyi kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kupata kura 15 na kumshinda Mhe. Rose Enock aliyepata kura 10 kati ya kura 25 zilizopigwa.
"Kwa mamlaka niliyopewa ninamtangaza mheshimiwa Elias Olenaigisa Molle kuwa Makamu Mwenyekiti aliyepata kura 15 na kumshinda mheshimiwa Rose Enock aliyepata kura 10 kati ya kura 25 zilizopigwa". Amesema Shoko.
Aidha Makamu Mwenyekiti huyo baada ya kutangazwa mshindi ameahidi kushirikiana na viongozi na wajumbe wote wa baraza hilo bila kujali tofauti zao za itikadi ya vyama ili kuhakikisha Mamlaka hiyo inathibitishwa na kuwa mamlaka kamili na hatimaye kuwa halmashauri inayojitegemea kwa kuwa inakidhi vigezo.
Hata hivyo Mhe. Mollel amesema kwa ushirikiano huo waliokuwa nao kwa kipindi chote cha miaka mitatu wamefanya kazi kubwa ya kuifikisha Mamlaka hiyo ya Ngaramtoni hapo ilipo licha ya changamoto nyingi zilizojitokeza tangu kuanzishwa kwake mwaka 20014.
"Nitaendelea kushirikiana na Mwenyekiti wangu na wajumbe wote wa baraza ili kuhakikisha Mamlaka hii inakuwa halmashauri inayojitegemea kwa manufaa ya wananchi wa Ngaramtoni bila kujali tofauti zetu za vyama" amesisitiza  Makamu Mwenyekiti huyo.
Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni  za serikali za mitaa uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa baraza la Mamlaka za miji midogo hufanyika kila baada ya mwaka mmoja na kufanya nafadi hiyo kugombewa kila baada ya muda huo kumalizika.
Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni ni mamlaka iliyo katika halmashauri ya Arusha na ilianzishwa rasmi mwaka 2014 ikiwa na kata saba na Vitongoji ishirini na tatu.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo
Loading...