Na. Elinipa Lupembe.
Wanawake wajasiriamali halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru, wameaswa kutumia fedha za mkopo walizopewa kwa malengo waliyoyakusudia wakati wa kuomba mkopo ili kuwarahisishia urejeshaji wa fedha walizokopa.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzie wakati wa kukabidhiwa mfano wa hundi mwenyekiti wa kikundi cha JADEKI kilichopo kata ya Kiranyi kinachojishughulisha na usindikaji mvinyo ndugu Juliana Mamuya amewaasa wanawake wenzie kuhakikisha fedha walizopewa wanazitumia kwenye biashara halisi walizozikusudia na kuziandika kwenye mchanganuo waliowasilisha wakati wa kuomba mkopo.
Mamuya amethibitisha kuwa kuna baadhi ya wanawake ambao baada ya kukabidhiwa fedha wanabadili mawazo ya biashara walizozikusudia kuziifanya na kuamua kuanzisha biashara nyingine tofauti jambo ambalo linasababisha kushindwa kurejesha fedha hizo kutokana na ugeni wa biashara wanazokurupuka nazo.
"Unakuta mwanamke ni mfugaji wa kuku anaomba mkopo kuongeza mradi wa kuku lakini akipokea pesa anaingiwa na tamaa na kununua toyo, siku mbili toyo imeibiwa mara imepata ajali ni dhahiri mtu huyu hawezi kufanya marejesho kwa wakati na kuingia kwenye mgogoro yeye na familia yake" amesema Mamuya
Amewaasa wanawake wenzake kuacha tamaa badala yake kusimamia biashara zao walizozoea kuzifanya kila siku jambo ambalo litawainua kiuchumi na kuwarahisishia urejeshaji wa fedha walizozikopa .
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mheshimiwa Idd Kimanta, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera amewataka wanawake hao kijikita kwenye shughuli zao za uzalishaji utakaowawezesha kurejesha fedha na kupata fursa ya kuchukua mikopo mingine na zaidi kutoa nafasi kwa makundi mengine kupewa mkopo.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Noah Lembris amewataka wanawake hao kutambua kuwa fedha hizo zinatokana na kodi mbalimbali wanazolipa na kurudishiwa asilimia kumi ya mapato hayo na kuwataka kutumia fedha hizo kujikwamua kiuchumi na kurejesha kwa wakati kwa kuwa mkopo sio zawadi.
Hata hivyo Afisa Maendeleo ya Jamii halmash
auri ya Arusha Angela Mvaa amewataka wanawake na vijana kujikita zaidi kwenye uanzishaji wa viwanda vidogo na uzalishaji wa malighafi za viwanda ili kuwenda sambamba na sera ya serikali ya viwanda.
Ameongeza kuwa kwa sasa serikali itajikita zaidi kutoa mikopo kwa wajasiriamali wenye kujishughulisha na viwanda vidogo pamoja na uzalishaji wa malighafi za viwanda. Aidha amesisitiza kuwa lengo la kutoa mikopo hiyo ni kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa kuwawezesha wananchi kujiajiri kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2020.
Halmashauri ya Arusha imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 220 kwa vikundi 43 vya wajasiriamalii, ikiwemo vikundi 38 vya wanawake na vikundi 5 vya vijana, fedha hizo ni asilimia 10% ya fedha za mapato ya ndani ya halmashauri.
Picha za Matukio wakati wa kupokea mikopo:
No comments:
Write comments