Tuesday, March 6, 2018

Wananchi wanaotumia barabara ya Mianzini -Timbolo wakiri kuanza kuyaona maendeleo nyumbani kwao



Na. Elinipa Lupembe.
    Wananchi wanaotumia  barabara ya  Mianzi - Timbolo iliyotengenezwa kwa kiwango cha lami wamekiri kuanza kuyaona maendeleo nyumbani kwao kwa kunufaika na barabara hiyo  ingawa imetengenezwa kwa umbali mfupi ukilinganisha na urefu wa barabara hiyo.   

      Wakizungumza na mwandishi wetu wakazi wa Mianzini eneo la kwa Loning'o wamethibitisha kuridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo na kudai kuwa tayari wameanza kuona mwanga wa maendeleo katika eneo lao.   
                   
        Wamesema kuwa uwepo wa lami katika barabara hiyo ni  neema kwao kwani wameisubiri lami hiyo tangu kuzaliwa kwao na kuongeza kuwa barabara hiyo imerahisisha usafiri kwa wakazi na wafanyabiashara  wanaosafirisha mazao kutoka maeneo ya mlimani na kuyaleta mjini.  

       Hata hivyo wakazi hao wameiomba serikali kuongeza umbali wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha  lami ifike mwisho na kuifanya barabara yote kuwa ni ya kiwango cha lami.    

    John Loshilu  mkazi wa Mianzini amethibitisha kupata neema hiyo ya barabara  kwa kusema kuwa wamenza  kuona maendeleo katika eneo lao ambayo hayajawahi kutokea tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.    
   
  " Awamu hii ya tano tumeanza kuyaona maendeleo, lami tulikuwa tunaiona mjini leo imefika katika eneo letu, kwa kweli hata kama haijafika mwisho lakini ni bora kuliko lile vumbi lilokuwa linatimka kwenye hii barabara" amesema Loshilu.   
  
       Barabara ya Mianzini - Timbolo yenye urefu wa takribani  Kilomita 9 imejengwa kwa kiwango cha lami urefu wa Mita 800  kwa gharama ya shilingi milioni 408 fedha za ambazo hutolewa na serikali kama ruzuku ya barabara.  
             
       Naye meneja wa TARURA Mhandisi  Kilusu  Teteana amesema kuwa  mpaka sasa wamemaliza hatua ya kwanza ya kutengeneza Mita 800  za barabara hiyo na  kuongeza kuwa wataendelea kutengeneza barabara hiyo na kuikamilisha kadiri fedha zitavyopatikana. 

       Hata hivyo mhandisi Kilusu amewataka wananchi hao kuitunza barabara hiyo kwa kuacha tabia ya kuelekeza mifereji ya maji kwenye barabara pamoja na kuendelea kutunza hifadhi za barabara.





No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo