Tuesday, January 9, 2018

Vilio na simanzi wateja wa benki tano zilizofutiwa leseni


Arusha/Bukoba. Wakati vilio na simanzi vikitawala kwa wateja wa Benki ya Meru Community (MecoB) wakitaka kujua hatima ya fedha zao baada ya benki hiyo kufutiwa leseni, Shirika la Maendeleo ya Wakulima (Mayawa) limeelezea mpango wake wa kufungua kesi mahakamani kutetea haki ya wanachama wake waliokuwa wamewekeza katika Benki ya Wakulima (KFCB).

Januari 4, benki hizo pamoja na nyingine za Efatha, Covenant na Njombe zilifutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na kuwa na mitaji midogo kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.

Wakizungumza na gazeti hili kwenye tawi kuu la MecoB, Usa River wilayani Arumeru waliokuwa wateja wa benki hiyo walisema jana kuwa kufungiwa kwa benki yao kumekuja wakati usio sahihi kwasababu wanahitaji fedha kwa matumizi mbalimbali. Mwalimu mstaafu Christina Mbisse alisema licha ya kununua hisa zenye thamani ya Sh600,000 ameweka akiba kwenye akaunti maalumu Sh12 milioni ambayo ni mirathi ya mtoto wake wa kike aliyemwachia watoto watatu wanaohitaji kulipiwa ada.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Anitha Haule alisema hajui hatma yake ya kuendelea na masomo kwa sababu benki hiyo ina akiba yake ya Sh5 milioni ambazo anazitegemea kwa ajili ya masomo. Naye meneja wa Mayawa, Charles Kamando alisema hatua hiyo imeathiri vikundi 278 vyenye wanachama zaidi ya 3, 000 waliokuwa na akaunti kwenye benki hiyo, hivyo watafungua kesi mahakamani.

Wilayani Missenyi, mweka hazina Saccos ya Kyaka, Wilson Wilbard alisema wamepanga kuitisha kikao cha dharura baada ya KFCB kufungwa huku wakiwa na akaunti iliyokuwa inatumika kwa ajili ya marejesho na kutoa fedha za kukopeshana.     


Source: Muungwana

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo