Na Elinipa Lupembe.
Wananchi wakazi wa kata ya Nduruma halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru wamejitolea kuchanga fedha za kujenga choo kwa ajili ya watumishi wa kituo chao cha Afya Nduruma baada ya watumishi hao kuzihama nyumba hizo kutokana na nyumba hizo kukosa vyoo.
Wananchi hao wamefikia uamuzi huo baada ya kuona tabu inayowakabili watumishi hao wanaolazimika kuishi mbali na kituo hicho na kusababisha utendaji wao wa kazi kulegalega jambo linalosababiszha pia upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi hao kusuasua.
Akizungumzia hatua hiyo, Kaimu Muuguzi Mkuu halmashauri ya Arusha Sista Agusta Komba amesema kuwa fedha hizo zimechangwa na wananchi wa Nduruma, watumishi wa idara ya Afya kwa kushirikiana na shirika la InGender Health na kupata kiasi cha shilingi milioni moja, kwa lengo la kufanikisha ujenzi wa choo hicho.
Sista Komba amefafanua kuwa wananchi wa Nduruma wamefikia hatua hiyo baada ya kufanya matembezi kituoni hapo na kujionea hali halisi ya nyumba za watumishi kituoni hapo.Ameongeza kuwa walifanya matembezi hayo kwa lengo la kuwamilikisha wananchi kituo hicho cha afya ili watambue kuwa kituo cha afya ni mali yao na kuweza kukitunza na kukihudumia kituo hicho cha afya.
" Tunataka wananchi kuvimiliki vituo vya afya na kutambua kuwa ni mali yao na si mali ya serikali kama wengi wanavyodhani, ila serikali ni msimamizi tu, lakini pia wananchi wafahamu huduma zote zinazopatikana kituoni hapo pamoja na mahitaji na changamoto zinazokikabili kituo chao na kuchangia kuzitatua" amesema Komba.
Naye Mganga mfawidhi wa kituo cha Afya Nduruma Dkt. Dorine Mushi amethibitisha kuwa nyumba za watumishi wa kituo cha Afya Nduruma ni chakavu kutokana na kujengwa muda mrefu na kusababisha watumishi kushindwa kuishi katika nyumba hizo jambo ambalo linaathiri utendaji kwa namna moja au nyingine
.
" Muuguzi akiishi karibu na eneo la kazi ni rahisi kutoa huduma kwa wagonjwa muda wote hata usiku wa manane tofauti na mtumishi anayeishi mbali na eneo la kazi" amesema Dkt. Mushi
Dkt. Mushi ameongeza kuwa choo hicho kinachojengwa ni muhimu kwa watumishi hao kwani ni aibu kwa binadamu kuishi kwenye nyumba isiyokuwa na choo na kuongeza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi huo na ukarabati wa nyumba watumishi hao watarudi kuishi hapo.
Hata hivyo serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 500 za ujenzi wa miundo mbinu ya kituo cha Afya Nduruma na kiasi cha fedha kitatumika kukarabati nyumba za watumishi na kufanya mazingira bora na rahisi kwa watumishi kutoa huduma.H
Halmashauri ya Arusha inawapongeza wananchi wa Nduruma kwa kujitoa kwa hali na mali kwa maendeleo ya Kata yao hasa kwa kuiunga mkono serikali yaO kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto.Aidha Uongozi wa Halmashauri ya Arusha unawataka wananchi wote ndani ya halmashauri ya Arusha na wadau mbalimbali kuiga mfano wa wananchi wa Nduruma kuchangia Maendeleo yao katika maeneo yao.
PICHA ZA CHOO NA NYUMBA ZA WATUMISHI ZITAKAZOFANYIWA UKARABATI.
Vyoo vilijengwa kwa nguvu za wananchi kwenye nyumba za watumishi wa kituo cha Afya. |
Nyumba ya Mtumishi wa kituo cha Afya Nduruma inategemewa kufanyiwa ukarabati na nyuma ni choo kilichojengwa kwa nguvu za wananchi. |
No comments:
Write comments