Na Sulbasia Evord
Timu ya Ulinzi na Usalama wa mtoto Halmashauri ya Arusha imepiga marufuku kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 kwenda kwenye kumbi za starehe nyakati za usiku.
Marufuku hiyo imetolewa wakati wa kikao chakupitia utekelezaji wa shughuli za ulinzi na usalama wa mtoto Halmashauri ya arusha kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2017/18
Hata hivyo timu hiyo inatekeleza sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2009 inayozuia kumtumia mtoto kwa shughuli yoyote inayofanyika kwenye kumbi za starehe hasa nyakati za usiku.
Aidha sheria hiyo imefafanua kuwa mtoto yoyote haruhusiwi kuingia kwenye kumbi za starehe kama klabu zinazopiga mziki nyakati za usiku.
Mwanasheria Martha limo ambaye ni mjumbe wa timu hiyo ameeleza kuwa jamii bado haijazingatia sheria hiyo kwakuwa bado jamii inatabia ya kuwatumia watoto kusimamia harusi na kukaa nao kwenye sherehe za harusi mpaka usiku wa manane na wengine kuingia kwenye klabu za disko bila kuzuiliwa.
Ameongeza kuwa sheria imeweka wazi adhabu ya kosa hilo nikifungo cha miezi 12 jela hivyo jamii inatakiwa kuchukua tahazari kabla ya kuingia kwenye mgogoro wa sheria hiyo.
Aidha amesema kuwa pamoja na kuwepo sheria hiyo lakini jamii inatakiwa ielimishwe kuhusu mazara makubwa yanayoweza kumpata mtoto katika kumbi za starehe iwe mchana au usiku.
"Sisi kama timu tunajaribu kutumia njia mbali mbali kuelimisha jamii mijini na vijijini kutambua athari za kisaikolojia zinazoweza kumpata mtoto anapoingia kwenye kumbi za starehe katika umri mdogo kwani athari yake huchua mda mrefu kujitokeza"amesema Martha.
Afisa Ustawi wa jamii halmashauri ya Arusha ndugu Mashaka Nkole ameeleeza mikakati ya halmashauri kukabiliana na tatizo hilo sugu ni pamoja na kutumia timu za ulinzi na usalama wa mtoto kwa ngazi ya kata kutoa elimu kwa jamii juu ya sheria ya kutoruhusu mtoto kuingia katika kumbi za starehe na kumbu za sherehe nyakati za usiku.
Ameongeza kuwa tayari Maafisa Watendaji wa kata wameandikiwa barua ya kuwataka kukabiliana na tatizo hilo katika maeneo yao pamoja na kutoa elimu kwa jamii husika.
Nkole ameendelea kufafanua kuwa jamii imekuwa na kawaida ya kuwatumia watoto kusimamia harusi na kwenda nao kwenye kumbi za sherehe zinazifanyika mpaka usiku wa manane jambo ambalo ni kosa kisheria.
" Hairuhusiwi kutumia watoto katika kumbi za sherehe hasa nyakati za usiku, kwanza ni kinyume cha maadili kwa baadhi ya mambo yanayofanyika hayaendani na umri wa watoto hao"amesema Nkole
Hata hivyo ameongeza kwa kusema kuwa wameandaa mkutano utakaohusisha viongozi wa Dini zote kwa lengo la kuwaeleza katazo hilo la kutoruhusu watoto kutumika kusimamia harusi na kwenda kwenye sherehe hizo.
Kadhalika kaimu Mwenyekiti Uchumi wa timu ya ulinzi na usalama wa mtoto Halmashauri ya Arusha Ndugu Nhojo Kushoka amewataka na kuwaomba wananchi wote na wakazi wa na wamiliki wa nyumba za starehe kushirikiana pamoja kuzuia watoto wenye umri chini ya miaka 18 kuingia katika kumbi za starehe nyakati za usiku.
"wasiruhusu watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kuingia katika vilabu vya pombe, kumbi za starehe na kumbi za harusi" amesema Kushoka.
PICHA ZA WAJUMBE WA TIMU YA ULINZI NA USAMA WA MTOTO WAKIWA KWENYE KIKAO CHA ROBO YA KWANZA 2027/2018
No comments:
Write comments