Na. Elinipa Lupembe.
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kata kumi na moja Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru wamepatiwa msaada wa biskeli 11 na makabati 11 kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Johs Snow Ink 'JSI' Kanda ya Kaskazini na kati linalojishughulisha na masuala ya Ulinzi na Usalama wa mtoto.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vitendea kazi hivyo Mkurugenzi wa JSI ndugu Antony Mwendamaka amesema kuwa shirika limefikia uamuzi huo baada ya kuona changamoto ya usafiri na utunzaji kwa kumbukumbu unaowakabili watendaji hao katika kutekeleza majukumu yao kwa kulinganisha na Jiografia ya maeneo yao.
Mwendamaka ameongeza kuwa lengo hasa la kutoa vifaa hivyo kwa watalamu wa ngazi za kata ni kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa watoto hasa watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na wale wenye ukinzani wa kisheria kwenye ngazi za kata, vijiji mpaka jamii.
" Uwepo wa vifaa hivi kwa pamoja vitawarahisishia kazi Maafisa hawa kwenye upatikanaji na utoaji wa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya watoto kwenye maeneo yao pamoja na utunzaji wa taarifa zao kwa kuwa kimaadili taarifa hizo za watoto ni taarifa za siri hazitakiwi kuwa wazi" amesema Mwendabaka
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo kwa kutambua umuhimu wa usafiri kwa watendaji hao kwa kuzingatia matatizo yanayowakabili watoto kwenye ngazi za kata na vijiji.
Aidha Dkt. Mahera amethibitisha kuwa halmashauri inakabiliwa na changamoto ya vyombo vya usafiri kwa watalamu wa ngazi za kata na vijiji na kiasi fulani kuathiri utoaji huduma kwa jamii hasa kwenye matukio ya ukatilikwa watoto matukio ambayo yanatokea ndani ya jamii kwenye maeneo ya kata na vijiji.
Aidha Dkt. Mahera amesema usafiri kwa watalamu wa ngazi za kata ni changamoto ambayo husababisha watalamu kushindwa kuwafikia walengwa kwa wakati hasa ukizingatia matukio ya ukatili kwa watoto wanatokea kwenye jamii ambazo zipo ndani ya vijiji na kata.
"Wakati mwingine watalamu wetu wanapata taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya watoto kutoka kwa wasamaria wema lakini wanashindwa kufika eneo la tukio kwa wakati jambo ambalo linasababisha kuvurugika hata kwa ushahidi wa tukio husika" amesema Dkt. Mahera .
Hata hivyo maafisa Maendeleo waliopokea vifaa hivyo licha ya kulishukuru Shirika la JSI kwa kuona changamoto zao na kuzitatua kwa vitendo wameahidi kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ari na kasi mpya na kuthibitisha kutumia mafunzo ya ulinzi na usalama wa mtoto waliyoyapata kwa urahisi zaidi.
Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Olkokola Agripina Chuwa amesema kuwa wanashukuru kupata vitedea kazi hivyo ambavyo kimsingi vitawarahisishia utendaji kazi hasa katika ufuatiliaji wa taarifa na matukio ya ukatili wa watoto katika maeneo yao ya kazi.
Aidha Chuwa ameelezea utofauti wa shirika la JSI na mashirika mengine ambayo yamekuwa yakiishia kuwapatia mafunzo bila kutoa vitendea kazi jambo ambali lilikuwa linakwamisha utekelezaji wa stadi walizokuwa wanapewa.
"Mashirika mengi yamekuwa yakitugharamia mafunzo mara kadhaa bila kutoa vitendea kazi jambo ambalo lilikuwa linatufanya kushindwa kutekeleza mbinu tulizozipata kwa shirika la JSI limekuwa tofauti wametoa mafunzo pamoja na vitendea kazi ambavyo vitatuwezesha kurahisisha utekelezaji wa kazi na kufikia malengo" amesema Chuwa
Awali vifaa hivyo vimetolewa kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kata za Ilkiding'a, Oljoro, Olkokola, Mwandeti, Oldonyowas, Oldonyosambu, Matevesi, Nduruma, Sokon II, Bwawani na Mlangarini.
Bwawani, Mlangarini, sokon 11, ilkidinga, oljoro,
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MAKABIDHIANO YA BAISKELI NA MAKABATI.
No comments:
Write comments