Wanawake wajasiriamali halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru wamekiri na kuthibitisha kuwa mikopo mingi inayotolewa na taasisi za fedha haiwainui wajasiriamali wadogo badala yake huwaumiza na kusababisha kushindwa kuendelea na biashara kutokana na masharti magumu ya mikopo hiyo.
Wajasiriamali hao wamesema hayo wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa vikundi vya wanawake na vijana vilivyokidhi vigezo na kutegemea kupata mikopo mapema wiki ijayo yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano Halmashauri ya Arusha.
Wameendelea kueleza kuwa kwa mjasiriamali mwenye mtaji mdogo ni ngumu sana kuendelea kwa kukopa kwenye mabenki na taasisi za fedha za fedha kutokana na taratibu za uendeshaji na urejeshaji wa mikopo yao.
Aidha wanawake hao wamesema kuwa wameamua kuachana kabisa na mikopo inayotolewa na benki na taasisi nyingine za fedha kutokana na masharti magumu yaliyowekwa na taasisi hizo ambayo huwa ni changamoto kubwa katika kurejesha mikopo wanayokopeshwa.
Wamefafanua kuwa dhamana ya mali zisizohamishika, riba kubwa pamoja na marejesho ya muda mfupi ni changamoto kwa wajasiriamali wadogo kiasi kushindwa kurejesha na kujikuta kwenye migogoro na taasisi hizo na baadaye kufilisiwa.
Ana kaaya mwanakikundi wa kikundi cha Mbunda kilichopo kata ya Kiranyi amesema kuwa alishindwa kuendelea na biashara yake baada ya kukopa benki na kushindwa kurejesha na kujikuta amefilisika hadi mtaji aliokuwa nao kabla ya kukopa.
"Riba kubwa ya mkopo na marejesho ya kila wiki yalinishinda kabisa na kujikuta nalazimika kuuza vitu vingine ili kulipa mkopo na kufilisika kabisa hadi mtaji niliokuwa nao" amesema Anna.
Hata hivyo Anna na wenzake wamesema kuwa wameridhishwa na masharti nafuu yanayotolewa na serikali kwa kukopeshwa vikundi vya wanawake na vijana na kuongeza kuwa mikopo hiyo inauwezo mkubwa wa kuwainua kiuchumi ukilinganisha na mikopo inayotolewa na Taasisi nyungine za kifedha.
"Tumeamua kujiunga vikundi na kujikita kwenye fursa ya mikopo inayotolewa na serikali yetu yenye riba ndogo na masharti rahisi ili tujiunue kiuchumi" wamesema wanawake hao
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Arusha Angela Mvaa amewataka wanawake na vijana hao kuachana na dhana ya VICCOBA badala yake kuanza kujikita kwenye uzalishaji zaidi hasa kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, ufugaji wa nyuki sekta ambazo zitawawezesha kuanzisha viwanda.
Ameongeza kuwa dhama za vikundi vya kuweka na kukopa zimepitwa na wakati serikali sasa inaelekeza nguvu kubwa kwenye vikundi vinavyojikita zaidi kwenye uzalishaji wa malighafi pamoja na viwanda vidogo.
"Niwashauri sasa kujikita kwenye uzalishaji wa malighafi pamoja na uanzishwaji wa viwanda, Unapokuwa na kiwanda ni fursa kubwa kwako na jamii nzima inayokuzunguka"amesema Mvaa
Mafunzo hayo ya siku moja yamelenga kuwaanda wajasiriamali hao kupokea mikopo, kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vidogo, uzalishaji wa bidhaa, utunzaji wa fedha pamoja na nidhamu ya mkopo ikiwemo matumizi sahihi ya mtaji, faida, mapato na matumizi.
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MAFUNZO HAYO.
No comments:
Write comments