Thursday, July 20, 2017

Jamii imetakiwa kutoa ushahidi kwenye kesi za ukatili wa kingono kwa watoto



Jamii imetakiwa kukubali kutoa ushahidi kwenye kesi za matukio ya ukatili kwa watoto pindi zinapofikishwa mahakamani kwa kuwa kesi nyingi zinakwama kutokana na kukosa ushahidi.
Hayo yamesemwa na Afisa Ustawi wa Jamii ndugu Beatrice Tengi wakati wa Mkutano wa Timu ya Ulinzi na Usalama ya Mtoto halmashauri ya Arusha wa robo ya mwisho kuanzia mwezi Aprili mpaka Juni, 2017 na kujadili taarifa za mwaka  mzima wa 2016/2017 uliofanyika kwenye Ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha.

Akiwasilisha taarifa ya matukio ya ukatili kwa mtoto kwa mwaka 2016/2017 Afisa Ustawi wa Jamii Tengi amesema kuwa jumla ya matukio 53 ya ukatili mbalimbali ya watoto yametolewa taarifa na watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kesi zinaendelea licha ya changamoto za ushahidi unaokwamisha kesi hizo kukamilika.

Afisa Ustawi huyo amedhihirisha kuwa timu ya Ulinzi na Usala wa mtoto imeonyesha mafanikio kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kuwa imachangia  ongezeko la upatikanaji wa taarifa za ukatili wa mtoto kitokana na timu hiyo kuwa na mikakati ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto.
"Tangu timu hii kuundwa imeleta mafanikio makubwa kutokana na kuelimisha jamii na watoto kufahamu haki zao na kumekuwa na mwamko mkubwa kwa jamii kuripoti matukio hayo.


Hata hivyo Tengi ameeleza kuwa licha jamii kuanza kutoa taarifa ya matukio hayo bado kuna changamoto kubwa ya ushahidi katika kesi hizo hasa kwa watoto waliofanyiwa ukatili wa kingono.

Aidha Tengi amefafanua kuwa ukatili wa watoto unafanywa na watu wa karibu kabisa kwa mtoto ikiwepo majirani,ndugu wa mtoto au jamaa wa mtoto jambo linalosababisha mahakama kushindwa kutolewa hukumu kutokana na ushahidi kushindwa kukamilika.

Naye mkuu wa Dawati la jinsia kituo cha Polisi USA WP Pendo Alex  amethibitisha kuwa kuna tatizo kubwa katika jamii kutoa ushahidi kwenye kesi zinazoletwa Polisi juu ya ukatili wa ngono kwa watoto kutokana na ushahidi kushindwa kukamilika kutokana na mahusiano kati ya mtuhumiwa na mtoto.

"Tunapata changamoto katika upelelezi wa kesi za ukatili kwa watoto kutokana na jamii kushindwa kutoa ushahidi kwa kuhofia uhusiano baina ya familia hizo" amesema WP Alex.

Mganga mkuu halmashauri ya Arusha Dk. Kazingo amesema kuwa ili kupata ushahidi wa mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono mtoto huyo asinawe mpaka afanyiwe vipimo licha ya kuwa watoto wenyewe wana uelewa mdogo kama kitendo walichofanyiwa ni kinyume na sheria.

Hata hivyo wajumbe wa kamati hiyo wamekubaliana kuendelea kutoa elimu kwa jamii umuhimu wa kuwalinda watoto kutokana na vitendo vya kikatili pamoja na kuelimisha watoto wenyewe kufahamu haki zao pamoja na kuandaa semina ya kuwajengea uwezo maafisa upelelezi, madaktari na waendesha mashitaka kwa ajili ya uendeshaji wa kesi za watoto ili watoto hao wapate haki zao.

Mkutano huo pamoja na shughuli za Timu ya Ulinzi na Usalama wa mtoto zinafadhiliwa na shirika lisilo la serikali la ACE AFRICA linalojishughulisha na masuala ya watoto ndani ya halmashauri ya Arusha.


No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo