Friday, July 21, 2017

Rais Magufuli kufunga Migodi yote

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Magufuli amesema kuwa atachukua uamuzi wa kufunga migodi yote iliyo chini ya wawekezaji ambao amewaita kuzungumza nao baada ya kubainika wizi katika Makinikia ya mchanga yaliyokuwa yakitoka katika migodi hiyo. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 50 kutoka Kibondo mpaka Nyakanazi Mkoani Kigoma ambapo amesema ni bora migodi hiyo ikagaiwa kwa watanzania ambao wanachimba na kulipa kodi kuliko kuwapa wawekezaji ambao hawalipo kodi pamoja na kuibia nchi. "Ni mara kumi migodi igawanywe kwa watanzania, wachimbe wenyewe tupate kodi kuliko hao wanaojiita wawekezaji, hawalipi kodi. Kama wawekezaji hao wangefuata utaratibu unaotakiwa ikiwemo ulipaji wa kodi ingesaidia kufanya maendeleo mengi nchini kwa kuboresha huduma zote za kijamii ikiwemo elimu na afya. Niwatake wananchi tusimamie kwa pamoja katika hili ili tuweze kutetea maslahi ya nchi yetu", amesema Rais Magufuli. Aidha Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa kuwa mkali na kuchukua hatua kwa wakandarasi wote waliopewa tenda endapo watabainika kufanya kazi zisizo na kiwango pamoja na wale ambao kazi zao zinakwenda taratibu na kulingana na muda wa ukamilisha kwa miradi ya maendeleo kwa wakati hasa katika ujenzi wa barabara.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo