Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni mheshimiwa Elias Munis ameonesha matumaini makubwa juu ya upatikanaji wa huduma ya Maji kwa wananchi na wakazi wa Mamlaka hiyo na vitongoji vyake ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2018.
Mwenyekiti huyo amesema hayo alipozungumza na mwandishi wetu mara baada ya kufunga Mkutano wa Baraza la Mamlaka hiyo la kujadili taarifa za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2017/18 .
Mwenyekiti Munisi amesema kuwa Mamlaka inamatumaini makubwa kuwa miradi ya maji inayotekelezwa katika mamlaka hiyo pindi itakapokamilika itapunguza adha ya maji inayowakabili wananchi wa Mamlaka hiyo kwa muda mrefu sasa.
Ameongeza kuwa kwa sasa kuna mradi wa maji inyotekelezwa ndani ya Mamlaka ikikamilika itaondoa adha ya maji na kufikia zaidi ya 80% ya wananchi kupata maji safi na salama.
Ameitaja miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji Ngaramtoni unaotekelezwa na Benki ya Afrika, miradi inayotekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani kwa kushirikisha nguvu za wananchi pamoja na mradi wa maji wa WaterAid ambaonuko katika hatua za awali kwa pamoja ikikamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Mamlaka.
Hata hivyo mwenyekiti Munis ameelezea changamoto ya ubovu wa miundo mbinu ya barabara katika Mamlaka hiyo na ameitaka Wakala wa babara TARURA kuongeza kasi ya matengenezo ya barabara kazi ambayo imeonekana kusuasua tangu kuanzishwa kwa TARURA.
Naye Mtendaji Mkuu Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni Bi. Sophia Shoko ameelezea changamoto inayorudisha nyuma maendeleo na kuhatarisha maisha ya wananchi wa Mamlaka hiyo ni pamoja na ujenzi holela unaosababisha maafa ya mara kwa mara wakati wa mvua na majanga ya moto.
Aidha Mtendaji huyo amewataka wananchi waliojenga kuta kwenye mikondo ya maji kubomoa ili kuruhusu maji kupita ili kuzuia mafuriko wakati wa mvua na kuwakumbusha wananchi kupata kibali kibali cha ujenzi kabla ya kuanza kujenga.
Aidha Mwenyekiti Munisi amewapongeza watalamu wa Mamlaka kwa kufanyakazi kwa bidii na kuhakikisha shughuli za maendeleo zinakwenda vizuri pamoja na kuwahudumia wananchi.
PICHA ZA MATUKIO YA MKUTANO WA BARAZA LA MAMLAKA YA MJI MDOGO NGARAMTONI.
No comments:
Write comments