Friday, July 7, 2017

Zaidi ya wakulima 400 wanufaika na elimu ya mbegu bora za maharage



Kupepeta-maharage

Zaidi ya wakulima mia nne kutoka wilaya saba wamenufaika kwa kupewa elimu ya matumizi ya mbegu bora za maharage ili kuweza kulima kilimo chenye tija ambapo itawasaidia kujikwamua na wimbi la umaskini.


Elimu hiyo imetolewa kutokana na wakulima wengi kuendelea kulima kilimo cha mazoea kisichofuata taratibu za kitaalamu na kwa kutumia mbegu ambazo hazikufanyiwa utafiti na mwishoni huishia kupata hasara.

Hayo yalisemwa na Meneja wa shamba la mbegu Arusha Marco Mwendo Katika siku ya wakulima wa zao la  maharage   walipotembelea shamba hilo eneo la Ngaramtoni linalosimammiwa na  wakala wa mbegu za kilimo Tanzania (ASA) .

Mwendo amesema kuwa lengo la maonesho hayo ni kuwakutanisha wakulima wa maharage pamoja na kuwapa elimu namna ya kuchagua mbegu bora za maharage pamoja na utaalamu wa kulima maharage bora kwa ajili ya mavuno mengi.

Alisema kuwa maonesho hayo yameendelea kuleta mafanikio makubwa kwa wakulima wa maharage kwa kuwa wakulima wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kutumia mbegu bora na kupata mafanikio makubwa katika zao la maharage.

"Kwa kweli tangu tumeanza kuleta wakulima hapa shambani  kujionea kilimo bora cha maharage tumeona mafanikio makubwa sana kwani wamekuwa wakilima kilimo chenye tija kwa kutumia mbegu bora tunazozalisha ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina".  alisema Mwendo. 

Aidha Mwedo amefafanua kuwa, shamba la mbegu Arusha lina ukubwa wa hekta 576,ambapo mbegu zinazozalishwa ni Mahindi, Maharage, Ngano, mbaazi na alizeti , mwaka jana walilima Hekta 391, pamoja na changamoto kubwa ya ukame na magonjwa yaliyojitokeza msimu uliopita, walifanikiwa kupata mbegu tani 115.

Alisema tani hizo  za mazao mbalimbali zote ziliuzwa kwa wakulima na makampuni binafsi ambapo msimu wa Mwaka 2016/17 wamelima Hekta 423 na matarajio yao yalikuwa ni kuvuna tani 273 za mbegu ikiwemo alizeti, maharage na mbaazi.

Kwa upande wa Mkurugenzi  Mtendaji wa halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera alisema kuwa, ni jambo zuri kuwaleta wakulima pamoja kwani inawasaidia kupata elimu ya kutumia mbegu zinazofaa kwa kujionea makampuni yanayozalisha mbegu pamoja na kupata utaalamu wa kilimo bora. 

Mahela aliwataka wakulima kutumia mbegu bora zilizofanyiwa tafiti na wataalamu ili kuwawezesha kuzalisha mazao mengi zaidi katika eneo kidogo tofauti na walivyokuwa wakitumia mbegu za mtaani ambazo Mwisho wa siku zinaishia shambani kutokana na kushambuliwa na magonjwa. 

"Tunawashauri wakulima kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti kwani ndio mbegu bora Kwa kilimo cha sasa kwani mkifanya hivyo itawasaidia kuongeza wingi Wa uzao Wa mazao yenu shambani" alisema mahera

Naye Mwakilishi wa kituo cha kimataifa kinachohusika na kilimo katika nchi za joto (CIAT),ambao ndio waandaji wa hafla hiyo  Jean -Claude Rubyogo  alisema kuwa, mradi huo wa kusaidia wakulima wa maharage umekuwa ukifadhiliwa na shirika la USAID  kupitia kituo hicho .

Alisema kituo chao  kitahakikisha wakulima wananufaika na mbegu bora zilizofanyiwa tafiti na kuwa mradi huo wataupeleka maeneo mingine ili wakulima wengi waweze kunufaike zaidi. 

 Maonesho hayo hufanyika kila mwaka na yamefanyika kwa mwaka wa tatu sasa tangu yaanzishwe kwa kushirikisha wakulima kutoka wilaya za Arumeru, Same, Siha, Hai, Hanang, na Mbulu ambapo wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima hao. 

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo