Na. Elinipa Lupembe.
Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI Selemani Jafo amewataka watumishi wa halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru kuacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea badala yake kufanyakazi kwa juhudi na maarifa na weledi ili kufikia malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi wa ngazi za chini.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa makao makuu ya halmashauri ya Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano wa halmashauri hiyo.
Waziri Jafo amesisitiza kuwa kila mtumishi anatakiwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kubuni mambo mbalimbali ambayo yataacha alama na historia katika halmashauri wanayoitumikia.
Jafo amesema kuwa watumishi wengi wa serikali wanafanya kazi kwa kubweteka kutokana na kuwa na ajira za kudumu tofauti na watumishi walioajiriwa kwenye sekta binafsi.
Amefananisha utumishi wa serikali na sekta binafsi na kusema kuwa watumishi wa sekta binafsi wanafanya kazi kwa kujituma sana kutokana na kuwa na ajira za mkataba ambazo huwalazimu kuwa wabunifu ili kujihakikishia ajira zao.
"Inasikitisha sana watumishi wa sekta binafsi wanafanya vizuri kuliko watumishi wa umma wakati wote wana elimu sawa na wamesoma vyuo pamoja, kuna tatizo la upimaji katika utumishi wa umma" amesema Waziri Jafo
Hata hivyo Waziri Jafo amewakumbusha watumishi hao kuwa wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kupata matokeo makubwa kwa taifa kwa kuwa wengi wao ni wasomi na wenye taaluma sawa na watumishi wa sekta binafsi.
Aidha amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha kushirikiana na wakuu wa Idara na Vitengo kwa kukaa mezani na watumishi mmoja mmoja kuandaa mpango kazi utakaopimwa mwishoni mwa mwaka.
Ameongeza kuwa imefika wakati wa mtumishi kupimwa kutokana na mpango kazi aliouandaa kwa kuangalia utekelezaji wake kwa mwaka mzima.
" Mtumishi atapimwa kutokana na mpango kazi utakaoonesha malengo aliyojiwekea aliyotekeleza, aliyoshindwa kutekeleza na sababu za kushindwa kutekeleza na kusisitiza fomu za Opras zijazwe na zikaguliwe kwa kukaa na mtumishi mezani" amesisitiza Waziri Jafo
Aidha amemuagiza mkuu wa mkoa kuanzisha kampeni ya kuondoa ya kuondoa alama sifuri kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita katika mkoa wa Arusha kwa kuwabana walimu kufundisha vizuri kwa kufuata na kumaliza silabasi.
Awali mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amemueleza Waziri Jafo mpango kazi wa mkoa wa Arusha wa kupandisha kiwango cha taaluma na idadi ya ufaulu kwa wanafunzi katika shule za sekondari na msingi mkoa wa Arusha.
PICHA ZA MATUKIO YA MKUTANO HUO
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri Jafo na watumishi wa makao makuu halmashauri ya Arusha. |
Watumishi wa Makao Makuu Halmashauri ya Arusha wakimsikiliza Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI alipozungumza nao kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo |
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mashaka Gambo akizungumza wakati wa kikao cha Waziri Jafo na Watumishi wa Halmashauri ya Arusha |
Watumishi wa halmashauri ya Arusha wakimsikiliza Waziri Jafo |
Watumishi halmashauri ya Arusha wakifuatilia mkutano |
No comments:
Write comments