Thursday, December 21, 2017

Naibu Waziri wa Afya amewataka wananchi kutosubiri kila kitu kifanywe na Serikali


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile amewataka wananchi kuacha tabia ya kusubiri kila kitu kifanywe na serikali wakati akishiriki kazi ya ujenzi wa shule ya msingi Chambasi Wilayani Kisarawe.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Dk. Ndugulile amesema kuwa kwa kipindi kirefu dhana ya wananchi kujitolea katika kufanya kazi za maendeleo imepungua kwa kiasi kikubwa na kuiachia Serikali ikitoa kila kitu kutekeleza miradi ya maendeleo hata kama inawezekana kazi hizo kutekelezwa na wananchi.

Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa kwa kipindi cha sasa cha Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa kazi tu wananchi hawana budi kujitoa katika kufanya shughuli za maendeleo katika maeneno yao ili kuisaidia Serikali na kujisaidia wao wenyewe kujiletea maendeleo.

“Msisubiri kila kitu kifanywe na Serikali vingine mnaweza kufanya weneyewe hongereni sana ninyi ni mfano wa kuigwa kwa vijiji vingine katika hili” alisema Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Chambasi, Bi. Fodia Makebu Tungaraza amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa shule umeibuliwa na wananchi wenyewe mara baada ya watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda kijiji cha jirani kuifata shule ya Msingi Msimbu takribani kilomita sita hivyo kuhatarisha maisha na usalama wa wanafunzi hao.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msimbu Bw. Hussein Mkambara ambae pia anayesimamia shule ya Chambasi hadi itakapopata usajili ameishukuru Serikali kwa kuona na kuwaunga mkono katika jiitihada za kujikwamua katika changamoto waliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu.

    No comments:
    Write comments

    Matangazo

    Matangazo