Thursday, December 21, 2017

Uchaguzi wa marudio kutumia Bilioni 3




 Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mesema kuwa jumla ya Sh bilioni 3.1 zitatumika kwenye uchaguzi wa marudiuo ambao kampeni zake zimeshaanza.

Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Januari 13 mwakani, kampeni zake zilianza tangu juzi kwa majimbo ya Singida Kaskazinina Longido wakati Jimbo la Songea Mjini kampeni zitaanza leo.

Kampeni hizo zitakamilika Januari 12 ikiwa ni siku moja kabla ya uchaguzi kufanyika. Akizungumza na HabariLeo jana, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima alisema kuwa gharama hizo zitahusu majimbo matatu na kata sita.

Wakati Tume ikieleza gharama hizo za Sh bilioni 3.1 za uchaguzi mdogo, jana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alinukuriwa akisema kuwa serikali imeokoa Sh bilioni 156 ambazo zingetumika kugharamia uchaguzi wa marudio endapo serikali ingeshindwa kesi 53 zilizofunguliwa kupinga matokeo ya ubunge wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Fedha hizo zimeokolewa kutokana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanikiwa kushinda kesi 52 na kushindwa kesi moja na hivyo kuokoa mabilioni hayo ya fedha. Akizungumzia uchaguzi katika majimbo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro ambayo pia yapo wazi kutokana na wabunge wake kujiuzulu, Kailima alisema mipango ya kuitishwa kwa uchaguzi ipo katika hatua za mwisho.

Alisema tayari NEC imeshapata barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ya kuieleza kuwa majimbo hayo yapo wazi na hivyo taratibu za kufanya uchaguzi wa marudio kwenye majimbo hayo zinaendelea. Alisema tume hiyo itakutana baadaye kutoa utaratibu kuhusu kufanyika kwa uchaguzi kwenye majimbo hayo mawili kwa kuwa kwa sasa wajumbe wengi wa Tume wako mikoani kikazi.

Alisema haitachukua muda mrefu utaratibu huo kutolewa kwani wanatarajia kukutana kati ya mwezi huu na Januari mwanzoni. Uhaguzi wa marudio kwa Jimbo la Longido unatokana na Maamuzi ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutengua ushindi wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Onesmo Ole Nangole.

Kwa Jimbo la Singida Kaskazini, uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa Mbunge Lazaro Nyalundu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujivua uanachama wa chama hicho pamoja na kujiuzulu ubunge wake na kujiunga na Chadema, wakati Jimbo la Songea Mjini uchaguzi unafanyika kutokana na aliyekuwa Mbunge jimbo hilo, Leonidas Gama kufariki dunia mwezi uliopita.

Jimbo la Kinondoni lipo wazi kufuatia aliyekuwa Mbunge wake, Maulid Mtulia (CUF) kujivua uanachama wa chama hicho na kujiuzulu nafasi zake ikiwemo ubunge Desemba 2, mwaka huu. Kwa jimbo la Siha aliyekuwa Mbunge wake, Dk Godwin Mollel naye alijivua uanachama wa Chadema na kujiuzulu nafasi zake zote ikiwemo ubunge na kujiunga na CCM hivi karibuni.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo