Tuesday, October 10, 2017

Tanga Cement yatoa mifuko ya Saruji kwa ajili ya Ujenzi nyumba za Polisi Arusha


Jeshi la Polisi mkoani Arusha limepokea  tani hamsini za saruji sawa na mifuko elfu moja yenye thamani ya shilingi milioni 12.5 toka kampuni ya Saruji yaTanga (Tanga Cement) kwa ajili ya  kusaidia ujenzi wa nyumba za Askari wa Jeshi hilo ambazo ziliteketea kwa na kusababisha jumla ya familia 13 kukosa makazi.

Akipokea shehena hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo ameishukuru Kampuni ya Tanga Cement kwa kujitoa na kutambua mchango wa askari katika kuimarisha usalama, na kuahidi kusimamia ili ujenzi huo kasi yake iongezeke.

Amesema kuwa mbali na kampuni hiyo pia amewaomba watu wengine binafsi pamoja na Makapuni mengine waige mfano toka kwa kampuni hiyo kuisaidia jamii hasa katika sekta mbalimbali kama vile elimu, afya  na majanga kama haya.

Kamanda Mkumbo pia alitumia fursa hiyo kushukuru watu binafsi , makampuni,  taasisi pamoja na majeshi ya Ulinzi na Usalama kama vile Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi Kilimanjaro, Chuo cha Polisi Moshi na Jeshi la Magereza.

Wengine ni kiwanda cha Magodoro cha Tanfoam, kiwanda cha A to Z, Ofisi ya Mwanasheria mkoani hapa, Green Valley School na Kampuni ya Otterlo Business Corporation Ltd (OBC) pamoja na watu binafsi ambao walitoa msaada wa fedha, Chakula, Saruji nguo pamoja na Magodoro.

Kwa upande wake Meneja Biashara wa kampuni hiyo Bw. Peet Brits alisema kwamba, wao kama kampuni wameweka mkazo kusaidia katika elimu, afya, maendeleo ya Jamii pamoja na mazingira lakini kwenye majanga mbalimbali kama vile ajali za moto.

Alisema kwamba anafahamu kazi zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kudumisha usalama ambapo unasaidia kuvutia mazingira mazuri ya kibiashara hapa nchini. Alisema wametoa msaada huo ili usaidie kujenga makazi ya familia za askari.

Bw. Brits alisema anajua walichochangia hakiwezi kutosheleza lakini wanaamini kitasaidia kwenye ujenzi wa nyumba hizo na kuzitaka kampuni pamoja na taasisi  kusaidia Jeshi la Polisi ambalo linaimarisha usalama hali ambayo inasaidia kuweka mazingira mazuri ya kibiashara.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo
Loading...