Kuelekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike duniani itakayoadhimishwa kesho, walimu wa shule zote za Msingi Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru wametakiwa kutumia muda walau wa dakika 40 kuzungumza na watoto wa kike juu ya haki, wajibu, pamoja na kujitambua thamani yao na kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa matukio ya ukatili na mtu yoyote, mazungumzo yatakayofanyika katika madarasa yao kwenye shule zao.
Maagizo hayo yametolewa na Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Arusha mwalimu Tumsifu Mushi wakati alipokutana na Waratibu wa Klasta, Maafisa Elimu Kata na walimu wakuu wa shule Msingi za serikali katika halmashauri hiyo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Creen Acres kuzungumzia changamoto zinazowakabili watoto wa kike katika halmashauri ya Arusha.
Mushi amesema kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kugundua tatizo linalowakabili watoto walioko shuleni kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili ndani ya familia na jamii zao pamoja na watoto kuchumbiwa wakiwa bado shuleni na kuwataka walimu kutumia siku ya kesho kuzungumza na watoto kwa kugawana walimu wa kike na watoto wa kike na walimu wa kiume na watoto wa kiume.
Amefafanua kuwa kuna ukatili mkubwa unaofanywa na jamii hasa wazazi dhidi ya watoto na zaidi kwa watoto wa kike ambao walimu tusipojipanga vizuri kugundua na kuufichua watoto tunaowafundisha hawatatimiza ndoto zao badala yake wataishia kuolewa na kuathirika kisaikolojia.
Mushi amewataka walimu hao licha ya kujipanga kupandisha kiwango cha taaluma shuleni lakini pia kila mwalimu ahakikishe anapanga muda kila wiki wa kuzungumza na watoto masuala ya kijamii pamoja na kuanzisha mabaraza ya watoto shuleni ambayo yatawapa watoto kujadili na kuzungumza mambo yanayowahusu ikiwemo changamoto zinazowakabili na namna ya kukabiliana nazo.
"Watoto wamejeruhiwa kutokana na mila na desturi za jamii zao hivyo ninyi walimu mkawe faraja ya watoto hawa kwa kuwafundusha, kuwaelekeza na kuwatolea taarifa za matukio ya kikatili wanayofanyiwa kwenye vyombo vya kisheria, walimu tukijitoa kwa hili nina hakika jamii iabadilika na watoto hawatakubali kunyanyasika" amesema Mushi .
Aidha Afisa Elimu huyo amewataka viongozi hao wa elimu kuhakikisha wanawafuatilia watoto katika shule zao na kubaini haraka endapo kuna mtoto aliyechumbiwa, mjamzito na anayefanyiwa ukatili wa aina yoyote na kutoa taarifa kwenye vyombo husika pamoja na kupanga muda wa kuzungumza wa wazazi na walezi ili watambue haki za mtoto na umuhimu wa mtoto kusoma.
Awali kikao kazi hicho kilihusisha Shitika lisilo la Kiserikali la ACE -AFICA na Center for Women and Children Development (CWCD) yanayojishughulisha na masuala ya kupambana na ukatili wa wanawake na watoto na ndoa za utotoni ambao kwa pamoja walitoa mada ya namna ukatili wa watoto unavyokatisha ndoto za watoto.
Mkurugenzi wa Shirika la CWCD Hindu Mbwego ametoa rai kwa walimu kushirikiana kupambana na ukatili wanaofanyiwa watoto wa kike kwenye familia zao kwa kukaa nao na kuzungumza nao kwa upendo ili watoto waweze kueleza namna wanavyonyanyasika kwenye familia zao.
Aidha amewataka pia kuwafuatilia watoto kwa kuwa wengine wamechumbiwa na kuandaliwa kuolewa mara baada ya kumaliza elimu ya msingi jambo ambalo ni kunyume cha sheria.
Naye mwalimu wa kujitolea kutoka shirika la ACE AFRICA Annemarrie Marshall amewataka walimu kutumia nafasi zao kumjengea mtoto uwezo ili aweze kutimiza ndoto zake kwa kuwa wananafasi kubwa endapo watazitumia vizuri.
Marshall amesisitiza kuwa majina mabaya wanayowaita watoto yananafasi kubwa ya kumjeruhi mtoto hivyo na kuathirika kisaikojoljia katika maisha yake yote, ameainisha majina hayo kama mjinga wewe, muongo, mpumbavu, mwizi, mvivu yanawaumiza watoto bila kujua amewata walimu pamoja na jamii kwa ujumla kuacha kutumia majina hayo kwa watoto badala yake kuwatia moyo pale wanapokosea.
Afisa Elimu kata ya Oloirieni mwalimu Digna Swai amekiri kufahamu zaidi juu ya malezi ya mtoto na kuwa kuna haki za mtoto ambazo mwalimu anapaswa kuzisimamia na kuhakikisha mtoto anapata faraja ambayo anaikosa nyumbani kutokana na ukatili anaofanyiwa kwenye familia.
Aidha mwalimu Swai amesema kuwa atahakikisha katika shule za kata yake kuanza kupunguza adhabu kwa watoto na kujipanga kuzungumza zaidi kwa upendo bila kutumia fimbo pamoja na kupanga siku za kuzungumza na watoto masuala ya ukatili kwa watoto tafauti na masomo na zaidi kuandaa utaratibu wa kuwa siku maalumu ya kuzungumza na wazazi juu ya usalama wa mtoto.
"Binfsi nimejifunza kitu kipya chenye uhalisia na tunakwenda kuanza kazi kesho ya kuwatambulisha watoto wanafunzi wetu Siku ya Mtoto wa Kike na tutaadhimisha kwa kukaa na watoto kujadili masuala ya usalama ya usalama wa mtoto wa kike na kujadili nao ukatili dhidi ya mtoto wa kike unaoendelea kwenye jamii, naamini tutapata mafanikio makubwa kwa mtoto wa kike" amesema Swai
Hata hivyo Afisa Elimu Mushi amewataka walimu kushirikiana na mashirika hayo kutoa elimu kwa watoto, wazazi, walei na jamii kwa ujumla kwa lengo la kumuokoa mtoto wa kike kukabiliana na ukatili unaomuandama katika maisha yake.
Picha za Matukio ya Kikao kazi hicho.
Waratibu Klasta, Maafisa Elimu kata na Walimu Wakuu wa shule za Msingi wakifuatilia na kusikiliza kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa juu ya usalama wa mtoto.
Mkurugenzi wa Shirika la CWCD Hindu Mbwego akiwasisitiza juu ya usalama wa mtoto
Mwalimu kutoka Shirika la ACE Africa Annemarrie Marshall akionysha picha ya msichana aliyejeruhiwa kutokana na kuitwa majina mabaya
Mwezeshaji wa Shirika la ACE AFRICA Goodila Joackim akitoa mada juu ya usalama wa mtoto
No comments:
Write comments