Sunday, August 20, 2017

Wanachama wa Simba SC wapitisha mfumo wa Hisa


Jumla ya wanachama 1,216 wa klabu ya Simba  wameridhia mfumo wa klabu hiyo kuuza Hisa baada ya Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC) jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Afya Jinsia na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala na kuhudhuriwa na wanachama na viongozi wa Klabu hiyo ulimalizika salama kwa wanachama kukubaliana kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo na wanachama wake kumiliki kupitia Hisa.


Kaimu Mwenyekiti wa klabu Salim Abdallah 'Try Again' amesema kuwa asilimia 50 ya hisa za Klabu ya Simba zitauzwa kwa mwekezaji yeyote au wowote watakaoungana wasiozidi watatu kwa sharti moja tu la kuwa wanachama wa klabu hiyo.


Abdallah amefafanua kuwa mwekezaji huyo au hao wanatakiwa kuweka dau lisilopungua Sh. Bilioni 20 ili kupatiwa asilimia 50 ya hisa za klabu na wakati huo wanachama wote wa Simba wamepewa asilimia 10 ya hisa za kuanzia.


Ameendelea kueleza kuwa asilimia nyingine 40 zitawekwa kama mtaji wa klabu na zitauzwa kwa wanachama baadaye, lakini wale wawekezaji walionunua asilimia 50 awali, hawataruhusiwa kununua hata hisa moja kwenye asilimia 40 za mtaji.

Baada ya mkutano huo kukamilika salama zoezi litakalofuata ni uhakiki wa wanachama wa klabu hiyo ili kuweza kujua mgawanyo wa asilimia 10 za hisa utakavyokuwa – na itaundwa Kamati maalum ya kupitia maombi ya wawekezaji wanaotaka kununua asilimia 50 ya hisa.


Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya Dk Kigwangala ameunga mkono mabadiliko hayo na kuwaambia wanachama wa Simba wamechelewa kufanya uamuzi wa mabadiliko hayo kwani walipaswa kufanya hivyo miaka mingi iliyopita na anaamini klabu nyingine zitafuata nyayo hizo.


“Leo Agosti 20 klabu ya Simba imetengeneza rekodi  nyingine baada ya ile ya mwaka 1977 ya kuwafunga Yanga 6-0, na sisi kama Serikali chini ya rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli tunaunga mkono mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu ya Simba,” amesema Dk. Kigwangala.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo
Loading...