Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angellah Kairuki
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) mhe. Angellah Kairuki, amesema katika kuwa kwa mwaka huu mpya wa fedha watumishi wote wa umma watakuwa wanalipwa mishahara kwa wakati mmoja ili kupunguza matatizo ya mishahara yanayojitokeza.Waziri Kairuki ametoa kauli wakati akizungumza na watumishi wa umma wa wilaya mpya ya Ubungo akiwa kwenye siku ya pili ya mwendelezo wa ziara yake katika halmashauri hiyo.
Waziri kairuki amesema kuwa awali watumishi wa umma walikuwa wanapata mishahara yao kwa nyakati tofauti lakini sasa wataingizia mishahara yao moja kwa moja katika akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) badala ya kupitia benki za biashara.
"Tunataka watumishi wote kupata mshahara kwa pamoja, hatutaki itokee huyu amewekewa mshahara tarehe 27, huku mwingine akienda kuangalia salio katika akaunti anaambiwa bado". amesisistiza Kairuki huku akishangaliwa na watumishi wa halmashauri hiyo.
Aidha Waziri Kairuki amefafanua kuwa lengo la serikali kuweka mfumo huo ni kuhakikisha watumishi wote wa umma wanapata mshahara wao kwa wakati mmoja na hiyo itasaidia Serikali kusimamia kwa umakini masuala ya mishahara.
Hata hivyo Waziri Kairuki amewataka waajiri kuwa makini kuthibitisha orodha ya majina ya watumishi wao kwa kuwa orodha wa watumishi watakaotakiwa kulipwa mishahara itawasilishwa kwa mwajiri wa sekta husika siku tatu kabla mshahara haujaingizwa katika akaunti ya mtumishi.
"Matumaini yangu waajiri watakuwa makini kuangalia orodha hizo ili isitokee hata mtumishi mmoja akaachwa," anasema Waziri Kairuki.
No comments:
Write comments