Advertisement

Thursday, March 8, 2018

Tumaini Jipya chachu ya maendeleo Arusha DC




Na. Elinipa Lupembe.

 Shirika lisilo la kiserikali la Tumaini Jipya lenye makazi yake kata ya Olkokola halmashauri ya Arusha limeonesha kuridhishwa  na utekelezaji wa shughuli za kuwahudumia wananchi  zinazofanya na halmashauri hiyo tangu kuanzishwa kwake.
      
              Akizungumza kwa njia ya mtandao mkurugenzi na mwanzilishi wa shirika hilo Bi. Louise Richardson raia wa Uingereza amesema kuwa ameridhishwa na utekeleza shughuli za kuwahudumia wananchi katika halmshauri ya Arusha kwa ili kutatua changamoto za huduma za kijamii zinazowakabili wananchi hasa wa maeneo ya vijijini.

         Louise ameoneshwa kuridhishwa zaidi na utekelezaji wa mradi wa maji wa vijiji vitano mradi ambo yeye binafsi ndiye chanzo cha upatikani wa ufadhili wa mradi huo kutoka nchini kwake Uingereza, baada ya kushuhudia adha ya maji wanaipata hasa watoto wakike wawapo shuleni na kuamua kurudi nchini kwao kutafuta fedha za kutekeleza mradi wa maji.

      Hata hivyo Louise amesema hayo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mkuu wa Kitengo cha huduma ya Jamii 'DFID' Bi.  Getrude Mapunda aliyetembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa maji mwishoni mwa wiki iliyopita, ameanza kuona upatikanaji wa huduma ya maji katika vijiji hivyo ambavyo kiuhalisia wana shida kubwa ya upatikani wa maji safi na salama.    
     
       Amesisistiza kuwa lengo hasa la shirika la Tumaini Jipya ni kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kuhakikisha huduma zote za jamii zinawafikia wananchi hasa waishio vijijini na kufafanua  kuwa endapo mradi huo utatekelezwa kwa wakati na kwa viwango na jamii kushiriki katika utunzaji na uchangiaji wa huduma za maji ili huduma hizo ziwe endelevu, serikali ya Uingereza itaendelea kutoa misaada mingi kupitia shirika lake la Tumaini Jipya.      
   
        Shirika la Tumaini Jipya limekuwa likifadhili shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo uwekaji vioo kwenye vyumba vya madarasa shule ya msingi Olbaki pamoja na kweka miundombinu ya umeme kwenye nyumba za walimu wa shule hiyo pamoja na zahanati ya kijiji cha Lengijave .   

        Licha ya misaada hiyo Louise ametoa msaada wa mashine ya kusaga nafaka ili kutatua changamoto inayowakabili wakazi wa kijiji cha Lengijave ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo, mradi  huo utakaoanza kufanya kazi mara baada ya mchakato wa kuingiza umeme kukamilika.
       
          Hata hivyo Louse amesema kuwa shirika la  Tumaini Jiya liko tayari kuendelea kutoa misaada mbalimbali ya kijamii kwenye sekta za elimu, afya na maji nchini Tanzania  kutokana na mapenzi mema aliyonayo hasa kwa wananchi wa kijiji cha Lengijave eneo ambalo amewahi kuishi kama 'volontia'.

         Bi. Louise   ambaye ni  Diwani nchini Uingereza,  ndiye chimbuko hasa la mradi wa maji wa vijiji vitano baada ya kukerwa na changamoto ya ukosefu wa  maji hasa kwa watoto wakike wawapo shuleni na kuamua kurudi nchini kwao kutafuta fedha,   Mradi wa maji wa vijiji vitano unafadhiliwa na serikali ya Uingereza kupitia wa na Idara ya Maendeleo ya kimataifa  'DFID' na kutekelezwa na shirika la WaterAid-  Tanzania.











Tuesday, March 6, 2018

Wananchi wanaotumia barabara ya Mianzini -Timbolo wakiri kuanza kuyaona maendeleo nyumbani kwao



Na. Elinipa Lupembe.
    Wananchi wanaotumia  barabara ya  Mianzi - Timbolo iliyotengenezwa kwa kiwango cha lami wamekiri kuanza kuyaona maendeleo nyumbani kwao kwa kunufaika na barabara hiyo  ingawa imetengenezwa kwa umbali mfupi ukilinganisha na urefu wa barabara hiyo.   

      Wakizungumza na mwandishi wetu wakazi wa Mianzini eneo la kwa Loning'o wamethibitisha kuridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo na kudai kuwa tayari wameanza kuona mwanga wa maendeleo katika eneo lao.   
                   
        Wamesema kuwa uwepo wa lami katika barabara hiyo ni  neema kwao kwani wameisubiri lami hiyo tangu kuzaliwa kwao na kuongeza kuwa barabara hiyo imerahisisha usafiri kwa wakazi na wafanyabiashara  wanaosafirisha mazao kutoka maeneo ya mlimani na kuyaleta mjini.  

       Hata hivyo wakazi hao wameiomba serikali kuongeza umbali wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha  lami ifike mwisho na kuifanya barabara yote kuwa ni ya kiwango cha lami.    

    John Loshilu  mkazi wa Mianzini amethibitisha kupata neema hiyo ya barabara  kwa kusema kuwa wamenza  kuona maendeleo katika eneo lao ambayo hayajawahi kutokea tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.    
   
  " Awamu hii ya tano tumeanza kuyaona maendeleo, lami tulikuwa tunaiona mjini leo imefika katika eneo letu, kwa kweli hata kama haijafika mwisho lakini ni bora kuliko lile vumbi lilokuwa linatimka kwenye hii barabara" amesema Loshilu.   
  
       Barabara ya Mianzini - Timbolo yenye urefu wa takribani  Kilomita 9 imejengwa kwa kiwango cha lami urefu wa Mita 800  kwa gharama ya shilingi milioni 408 fedha za ambazo hutolewa na serikali kama ruzuku ya barabara.  
             
       Naye meneja wa TARURA Mhandisi  Kilusu  Teteana amesema kuwa  mpaka sasa wamemaliza hatua ya kwanza ya kutengeneza Mita 800  za barabara hiyo na  kuongeza kuwa wataendelea kutengeneza barabara hiyo na kuikamilisha kadiri fedha zitavyopatikana. 

       Hata hivyo mhandisi Kilusu amewataka wananchi hao kuitunza barabara hiyo kwa kuacha tabia ya kuelekeza mifereji ya maji kwenye barabara pamoja na kuendelea kutunza hifadhi za barabara.





Monday, March 5, 2018

Jamii imetakiwa kutunza miundo mbinu ya maji inayotengenezwa kwa gharama kubwa


Na. Elinipa Lupembe.

Jamii imetakiwa kushiriki kwa hali na mali kutunza rasilimali maji pamoja na kusimamia miundo mbinu ya maji inayojengwa kwenye maeneo yao kwa kuwa inajengwa kwa gharama kubwa zaidi  ili miradi ya maji inayojengwa iwe endelevu kwa miaka mingi ijayo.    

         Rai hiyo imetolewa na mkuu wa Idara ya huduma za Jamii Idara ya Maendeleo ya Kimataifa  Uingereza 'DFID', Bi. Getrude Mapunda alipokutana na viongozi wa jamii kutoka eneo linalotekelezwa mradi wa maji wa vijiji vitano ndani ya halmashauri ya Arusha maarufu kama mradi wa maji wa WaterAid unaofadhiliwa na Idara ya Maendeleo ya nchini Uingereza 'DFID' kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5.     

      Mapunda amekutana na viongozi hao ili kuthibitisha ushirikishwaji wa jamii katika utekelezaji wa mradi huo ambao tayari miundo mbinu yake imeanza kuchimbwa na unategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa 2018.   

         Licha ya kuridhishwa na uelewa wa pamoja waliokuwa nao viongozi hao baada ya kujengewa uwezo  juu ya mradi huo wa maji, Mapunda amewataka viongozi hao kuendelea kuweka mikakati thabiti ya utunzaji wa mazingira ambayo ndio chanzo kikuu cha upatikanaji wa rasilimali maji.        
   
        Aidha amendelea kufafanua kuwa miradi ya maji inatumia gharama kubwa kujengwa hivyo jukumu kubwa la wananchi ni kuwa na mikakati thabiti ya kuitunza na kuiendeleza miradi hiyo ili iweze kutumika kwa miaka mingi ijayo na vizazi vijavyo.   

      "Ili mradi wa mji uwe endelevu ni jukumu la jamii kutunza  miundo mbinu ya maji ikiwemo kuchangi gharama za maji kwa ajili ya maintainance pamoja na kutunza mazingira ya uhifadhi wa maji" amesema Mapunda.     
                               
          Naye mhandisi wa maji mkoa w Arusha Mhandisi Makaidi amethibitisha hali halisi ya kupungua kwa kiasi cha  maji inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi na kusababisha maji kupungua na kupatikana  kwenye kina kirefu kadiri siku zinavyokwenda tofauti na miaka ya nyuma.     
   
   Amefafanua kuwa suala la utunzaji wa mazingira linapaswa kupewa kipaumbele na jamii nzima ili kuepuka madhara makubwa ya ukosefu wa maji yanayoweza kutokea kwa  siku za baadaye. 

    "Tafiti zinaonesha kwa sasa maji yanapatikana urefu 
wa mita 100 mpaka 150 kwenda chini,  kama tusipochukua hatua madhubuti miaka kumi mpaka ishirini ijayo maji hayo yatapatikana kina cha mita 200 mpaka 300 jambo ambalo litaathiri hata miradi hii inayotekelezwa sasa" amesisitiza Mhandisi Makaidi. 
             
    Hata hivyo viongozi wa jamii wa eneo la mradi wamethibitisha kuunga mkono juhudi za serikali za utunzaji wa mazingira, utunzaji wa miundo mbinu ya maji pamoja na uchangiaji wa gharama za huduma za maji ili kuendeleza miradi hiyo ya maji ambayo  serikali na  wafadhili hutumia gharama kubwa kuijenga.  
                     
       Wameongeza kuwa katika maeneo yao kumekuwa na agenda ya kudumu ya utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi za familia na jamii nzima kwa kuhamasisha wananchi kutunza mazingira.     

       Diwani wa kata ya Olkokola mheshimiwa Kalanga Laizer amesema kuwa wananchi wa kata yake wamehamasika kujenga vyoo bora baada ya kuwa na mkakati wa kutoza faini kwa nyumba isiyokuwa na choo  bora na muitikio ni mkubwa kwa sasa.       

    "Kwa sasa wananchi wa kwetu wana vyoo bora licha ya kuwa bado kuna changamoto ya maji katika maeneo hayo lakini tunaamini mradi huu ukikamilika shida itakwisha. Amesema Mheshimiwa Kalanga.

     Mradi huo wa maji unatekelezwa kwenye vijiji vya Olkokola na Lengijave na vitongoji vya Olmotonyi, Ekenywa na Seuri vya Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 kwa ufadhili wa serikali ya Uingereza kupitia Idara ya Maendeleo ya  Kimataifa  'DFID'.

       Wakati huo huo serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeongeza kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya ujenzi wa mradi huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwezesha kutumia chanzo cha maji cha Emutoto kilichopo kwenye msitu ndani ya hifadhi ya mlima Meru licha ya mradi huo kutumia vyanzo hivyo viwili vya kuchimbwa.

        Mradi huo unategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa  2018 na unategemewa kuhudumia takribani watu 50,000 ambao watapata maji ndani ya mita 400 na kutekeleza mpango wa serikali ya awamu ya tano wa kuhakikisha asilimia 90% ya wakazi wa vijiji kupata maji safi na salama ifikapo mwaka 2025.






Wednesday, February 21, 2018

Wanawake waaswa kutumia fedha za mikopo kwa malengo waliyoyakusudia





Na. Elinipa Lupembe.
Wanawake wajasiriamali halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru, wameaswa kutumia fedha za mkopo walizopewa kwa malengo waliyoyakusudia wakati wa kuomba mkopo ili kuwarahisishia urejeshaji wa fedha walizokopa.   
    
        Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzie wakati wa kukabidhiwa mfano wa hundi  mwenyekiti wa kikundi cha JADEKI kilichopo kata ya Kiranyi kinachojishughulisha na usindikaji mvinyo ndugu Juliana Mamuya amewaasa wanawake wenzie kuhakikisha fedha walizopewa wanazitumia kwenye biashara halisi walizozikusudia na kuziandika kwenye mchanganuo waliowasilisha wakati wa kuomba mkopo.     

         Mamuya amethibitisha kuwa kuna baadhi ya wanawake ambao baada ya kukabidhiwa fedha wanabadili mawazo ya biashara walizozikusudia kuziifanya na kuamua kuanzisha biashara nyingine tofauti jambo ambalo linasababisha kushindwa kurejesha fedha hizo kutokana na ugeni wa biashara  wanazokurupuka nazo.  
  
       "Unakuta mwanamke ni mfugaji wa kuku anaomba mkopo kuongeza mradi wa kuku lakini akipokea pesa anaingiwa na tamaa na kununua toyo, siku mbili toyo imeibiwa mara imepata ajali ni dhahiri mtu huyu hawezi kufanya marejesho kwa wakati na kuingia kwenye mgogoro yeye na familia yake"  amesema Mamuya   

               Amewaasa wanawake wenzake kuacha tamaa badala yake kusimamia biashara zao walizozoea kuzifanya kila siku jambo ambalo litawainua kiuchumi na kuwarahisishia urejeshaji wa fedha walizozikopa .       
     
         Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mheshimiwa  Idd Kimanta,  Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera amewataka wanawake hao kijikita kwenye shughuli zao za uzalishaji utakaowawezesha kurejesha fedha  na kupata fursa ya kuchukua mikopo mingine na zaidi kutoa nafasi kwa makundi mengine kupewa mkopo.  
    
       Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Noah Lembris  amewataka wanawake hao kutambua kuwa fedha hizo zinatokana na kodi mbalimbali wanazolipa na kurudishiwa asilimia kumi ya mapato hayo na kuwataka kutumia fedha hizo kujikwamua kiuchumi na kurejesha kwa wakati kwa kuwa mkopo sio zawadi.      
       Hata hivyo Afisa Maendeleo ya Jamii halmash
auri ya Arusha Angela Mvaa amewataka wanawake na vijana kujikita zaidi kwenye uanzishaji wa viwanda vidogo na uzalishaji wa malighafi za viwanda ili kuwenda sambamba na sera ya serikali ya viwanda.

         Ameongeza kuwa kwa sasa serikali itajikita zaidi kutoa mikopo kwa wajasiriamali wenye kujishughulisha na viwanda vidogo pamoja na uzalishaji wa malighafi za viwanda.    Aidha amesisitiza kuwa lengo la kutoa mikopo hiyo ni kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa kuwawezesha wananchi kujiajiri kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2020.      

         Halmashauri ya Arusha imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 220 kwa vikundi 43 vya wajasiriamalii, ikiwemo vikundi  38 vya wanawake na vikundi 5 vya vijana, fedha hizo ni asilimia 10% ya  fedha za mapato ya ndani ya halmashauri.

Picha za Matukio wakati wa kupokea  mikopo:





















Tuesday, February 20, 2018

Wananchi Arusha DC watakiwa kutambua umuhimu wa kulipa kodi na ushuru elekezi


Wananchi wakazi wa halmashauri ya Arusha wametakiwa kutambua umuhimu wa kulipa ushuru na kodi mbalimbali elekezi na kufahamu kuwa mapato hayo hutumika  kwenye shughuli za maendeleo katika maeneo yao na taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na wajumbe wa Baraza la waheshimiwa madiwani wakati wa mkutano wa Baraza hilo wa kujadili taarifa za maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa halmashauri hiyo.

Madiwani hao wametoa rai hiyo wakati wa kujadili agenda ya kupitisha mapendekezo ya sheria ndogo za ushuru wa halmashauri hiyo kwa lengo la kukusanya mapato ya ndani agenda iliyokuwa na mijadala yenye mivutano mingi.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Noah Lembris amesema kuwa ifike wakati kila mwananchi  kutambua umuhimu wa kulipa kadi na ushuru na kutambua kodi hizo hukusanywa kwa ajili ya maendeleo ndani  ya halmashauri yao.

Ameongeza kuwa halmashauri inaendeshwa kwa mapato ya ndani yanayotokana na kodi na ushuru unaotozwa kwa wananchi na kuongeza kuwa asilimia sitini ya mapato hayo yanarudi kwenye kata na vijiji kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

" Kodi na ushuru unaokusanywa kwenye maduka, masoko na maeneo mbalimbali zinatumika kuendesha halmashauri na asilimia sitini inarudi vijijini kutekeleza shughuli na miradi ya maendeleo kwa faida ya wananchi wenyewe hivyo ni vema wananchi kulipa bila kukwepa" amesema Mwenyekiti Lembris

  Naye Diwani wa kata ya Musa Mheshimiwa Florah Zelothe amesema kuwa hakuna namna halmashauri inaweza kuendeshwa bila kuwa na mapato hivyo ni vema waheshimiwa madiwani kuwaelimisha wananchi kuwa na tabia ya kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo katika maeneo yao.

Awali Madiwani hao katika mkutano huo licha ya kupitia mapendekezo ya Sheria hizo za Ushuru wamejadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha miezi mitatu na kuweka mipango mikakati ya utekelezaji wa shughuli hizo kwa robo ijayo ya tatu.






caption









Matangazo

Matangazo