Na. Elinipa Lupembe
Akizungumza na mwandishi wetu Mganga Mkuu Halmashauri ya Arusha Dkt. Omari Sukari amesema kuwa mara baada ya kituo hicho kukamilika kinategemea kuhudumia zaidi ya watu 14,000 na kaya 3,894 kutoka kata ya Nduruma na kata za jirani za Mlangarini na Bwawani na vijiji jirani vya mkoa wa jirani wa Manyara.
Idadi hiyo ya watu inatokana na kata hizo kutokuwa na kituo kingine cha Afya na kuongeza kuwa kituo hicho ni mkombozi kwa wananchi wa maeneo hayo kwa kuzingati uhitaji wa huduma za afya kwa jamii hizo.
"Ni dhahiri kituo hiki ni mkombozi kwa wakazi wa maeneo haya kutokana na kata za jirani za Mlangarini na Bwawani kutokuwa na kituo kingine cha afya kituo hiki kintegemea kitatoa huduma kwa wananchi wote wa maeneo hayo" amesema Dkt. Sukari
Mganga huyo ametaja miundo mbinu inayojengwa sasa ni pamoja na Wodi ya mama na mtoto, maabara, jengo la kujihifadhia maiti, nyumba ya mtumishi, jengo la upasuaji, kichomea taka, eneo la kufulia nguo na ukarabati wa majengo ya zamani.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera amesema kuwa serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya kituo hicho cha afya na tayari imekamilika kwa zaidi ya asilimia 70.
Aidha Kituo cha Afya Nduruma kimewekwa Jiwe la Msingi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Selemani Jafo mapema wiki hii wakati wa ziara yake ya siku moja na kuahidi kuendelea kutoa mahitaji muhimu ya kituo hicho ikiwemo gari la wagonjwa kadiri fedha zitakavyopatikana.
Akizungumzia ujenzi huo Dkt. Mahera amesema kuwa ujenzi huo umwekwenda kwa kasi kubwa kutokana na matumizi ya Force Account kwa kutumia local fundi pamoja na usimamizi wa moja kwa moja wa Idara ya Ujenzi ya halmashauri kwa kushirikiana na kamati ya ujenzi ya Kijiji tofauti na wangetumia mkandarasi.
Hata hivyo Mkurugenzi Mahera ametaja neema nyingine ya umaliziaji wa ujenzi wa kituo cha Afya Manyire kata ya Mlangarini unaotegemea kuanza mapema mwaka huu baada ya kupata ufadhili kutoka serikali ya Japani.
Ameongeza kuwa serikali ya Japani kupitia ubalozi wa wake nchini Tanzania imetoa kiasi cha shilingi milioni 200.2 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo cha Afya Manyire ambacho awali kilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi wa kata ya Mlangarini.
" Tuliandika andiko ubalozi wa Japan nchini Tanzania la kuomba kumalizia ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa bahati nzuri walikubali kutoa kiasi hicho cha fedha na mchakato umeshakamilika muda mfupi ujao ujenzi utaanza" amesema Mkurugenzi Mahera
Aidha Dkt. Mahera ameongeza kuwa halmashauri ina mikakati ya kutafuta fedha kwa kushirikisha wananchi pamoja wadau wa ndani na nje ya nchi ya kuhakikisha kila kata ndani ya halmashauri inakuwa na kituo cha afya chenye hadhi ya nyota tano.ñ
No comments:
Write comments