Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imeanika majina 57 ya kampuni, shule, vyuo na mashirika ambayo waajiri wake hawawasilishi makato ya wanufaika wa mikopo kwa wakati.
Uanikaji wa majina hayo kupitia tovuti ya HESLB umekuja siku mbili baada ya kutangaza kufanya hivyo Jumatano iliyopita.
Mkurugenzi Msaidizi Urejeshaji Mikopo, Phidelis Joseph alisema kabla ya kuanza kuwasaka wanufaika 119,497 ambao hawajarejesha mikopo yao, wataanika majina yao hadharani.
Miongoni mwa kampuni zilizotajwa ni pamoja na Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la NSSF, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Puma Energy Limited, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Zipo pia shule za sekondari ambazo waajiri wake hawapeleki fedha kwa wakati licha ya kuwakata wafanyakazi wao.
Akifafanua kuhusu muda wa kuwasilisha fedha za makato ya wanufaika, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema kila mwajiri ana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha makato ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kwa Bodi ndani ya siku 15 baada ya mwisho wa mwezi.
“Baadhi ya waajiri wamekuwa hawafanyi hivyo na kuilazimisha Bodi ya Mikopo kuanza kuwasaka kwa nguvu.
“Katika msako huu hatutamuacha mtu au mwajiri yeyote anayekiuka sheria iliyoanzisha Bodi,” alisema Badru.
Kaimu Mkurugenzi wa Habariwa HESLB, Omega Ngole alisema kwamba idadi ya wanaokwenda kulipa madeni yao imeongezeka.
Alisema kwa kawaida ofisi zao za kanda zilizopo Arusha, Dodoma, Mwanza na Zanzibar hupokea wadaiwa wapya kati ya 15 hadi 25 kwa siku, lakini kuanzia jana wamepokea zaidi ya 50.
Akizungumzia zaidi kuhusu ofisi za makao makuu, Ngole alisema: “Tunapokea wadaiwa wapya wanaotaka kulipa zaidi ya 300 ambayo haikuwa kawaida, wapo na viongozi ambao majina yao yapo kwenye orodha ya wadaiwa, wamemaliza leo.”
Alisema kwamba wanawashukuru wote kwa kutimiza wajibu wao kwa kuwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuwasomesha wahitaji wengine.
No comments:
Write comments