Sunday, July 9, 2017

TFF yatoa Kongole kwa Uongozi wa Soka la Wanawake



Kaimu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amewapa kongole viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake (TWFA), waliochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Chichi, Dar es Salaam.

Katika Uchaguzi huo Amina Karuma aliyegombea kutetea kiti chake aliibuka kidedea kwa kupata kura 47 kati ya 52 za wapigakura wote huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikichukuliwa na Rose Kissiwa ambaye aliyepata kura 42, uchaguzi uliopata uwakilishi wa theluthi mbili ya mikoa yote ya Tanzania.

Somoe Ng'itu mwanahabari Mkongwe wa Gazeti la Nipashe kutoka Jumba la Magazeti la The Guardian, aliibuka nafasi ya Katibu Mkuu kwa kujizolea jumla ya kura 49 huku Theresia Mung’ong’o alishinda nafasi ya Katibu Msaidizi.

Nafasi ya Mweka Hazina wa TWFA linyakuliwa na Hilda Masanche aliyepata kura 25 wakati Mwanahabari mwingine Zenna Chande alishinda nafasi ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kupata kura 44.

Wajumbe Triphonia Temba, Mwamvita Kiyogoma, Jasmine Soudy na Chichi Mwidege hawakushinda baada ya wagombea wote wanne kutopata zaidi ya nusu ya kura kulingana na idadi ya wapigakura kwa mujibu wa katiba ya TWFA.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Wakili Msomi George Mushumba, ambaye pia hakusita kuwapongeza washindi washindi wote.

Akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi aliwataka wajumbe hao kuwa makini katika kuchagua na kwa kuwa huu si wakati wa kufanya mzaha katika soka la wanawake.





No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo