Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Idd Kimanta ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Monduli amepokea msaada wa madawati 740 kwa shule 13 za Wilaya ya Arumeru zinazozunguka shamba hilo kwa lengo la kutatua changamoto ya upungufu wa madawati unaozikabili shule hizo.
Msaada huo wa madawati umetolewa na Uongozi wa Shamba la Miti la Meru-Usa ikiwa ni mchango wa shamba hilo kwa jamii inayozunguka shamba hilo pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha shule zote zina madawati ya kutosha kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa kwa sasa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo meneja wa Shamba la miti Robert Faustine amesema kuwa wameamua kutoa madawati kwa shule hizo kwa kuwa zinaupungufu mkubwa wa madawati ukilinganisha na idadi ya wanafunzi na baadhi ya shule hizo kuwa ni mpya.
Ameongeza kuwa ofisi inatambua upungufu wa madawati kwenye baadhi ya shule zinazozunguka shamba hivyo na kuahidi kueendelea kushirikiana na taasisi nyingine kutatua tatizo hilo.
Hata hivyo Faustine amesema kuwa kati ya shule hizo 13 kila shule imepata madawati 56 na kuzitaja shule hizo ni pamoja na shule ya msingi Lemong'o, Ngedeko, Lesakata Farm, Olmotonyi, Oldonyowas, Sambasha na Olkokola za Halmashauri ya Arusha na shule za Urisho, Sangananu, Ngongongare na Sakila za Halmashauri ya Meru.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru ameshukuru kwa msaada huo na kuwataka walimu kahakikisha wanasimamia vema utunzaji wa madawati hayo pamoja kufundisha kwa bidii na kuongeza kiwango cha ufaulu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera licha ya kushukuru kwa msaada huo amesema kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa halmashauri iko katika mchakato wa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa madarasa ya kwanza na awali pamoja na wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na kuwa bado kuna upungufu wa madawati na vyumba vya madarasa.
Dkt. Mahera amewaomba wadau wengine kujitokeza kuchangia madawati pamoja na vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kukamilisha vyumba vya madarasa changamoto inayotokana na ongeeko la wanafunnzi shuleni kutokana na sera ya elimu bila malipo.
No comments:
Write comments