Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii - CHF ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu pindi wanapougua wao na familia zao.
Ametoa rai hiyo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utoaji wa huduma za afya pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kituo cha Afya Nduruma na kuzungumza na wananchi na wafanyakazi wa kituo hicho.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa serikali imeanzisha mfuko wa Afya ya jamii 'CHF' na imeshaweka mikakati thabiti ya kuhakikisha wanachama wote wa mfuko huo wanapata matibabu na dawa zote muhimu bila usumbufu wowote na katika vituo vyote vya afya.
Ameongeza kuwa serikali inaandaa utaratibu ambao wananchi kujiunga na bima za afya itakuwa ni lazima na si hiari tena hivyo wananchi wanapaswa kuanza kuzoea kujiunga na mfuko hiyo sasa.
"Kiuhalisia gharama za matibabu ni kubwa sana kwa mwananchi wa kawaida kumudu, na ugonjwa nao unakuja ghafla ukiwa huna pesa wala kujiandaa hivyo ukiwa na bima ya Afya inarahisisha, ni bora kujiunga ili kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote" amesema.
Dkt. Ndugulile amewaagiza viongozi wa vitongoji, vijiji, kata kwa kushirikiana na Diwani wa kata ya Nduruma kuongeza kasi ya kuwahamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii na kuongeza kuwa gharama ya shilingi elfu kwa kaya ya watu sita kwa mwaka ni ndogo sana hakuna mwananchi anaweza kushindwa kumudu.
Aidha amewataka watumishi wa vituo vya Afya kutumia fedha za CHF kununua dawa na vifaa tiba kwa kuwa dawa zote muhimu zinapatikana kwenye Bohari ya Dawa 'MSD' na kuacha kuhifadhi fedha hizo kwenye akaunti.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya kituo hicho na kusema kuwa amejihakikishia ubora wa majengo kwa kulinganisha na thamani ya fedha zilizotumika.
Amefafanua kuwa matumizi ya 'Force Account' yameonyesha mafanikio makubwa ukilinganisha na kutumia Mkandarasi na kuwataka wananchi Kamati ya Ujenzi kuendelea kushiriki na kufuatilia hatua zote za ujenzi na manunuzi ya vifaa vyote kwa kuwa fedha hizo ni zao.
Awali Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Nduruma Dkt. Dorine Moshi amesema kuwa kituo kilipokea shilingi milioni 500 kutumia Force Account kupata fundi wa kujenga na mpaka sasa zimetumika milioni 115 na majengo yamefikia hatua ya kupauliwa.
Ameyataja majengo yaliyojengwa ni pamoja na maabara, jengo la uzazi 'Maternity ward', chumba cha kuhifadhia maiti'mortuary' na nyumba ya daktari na kuongeza kuwa bado fedha hizo zitatumika kujenga kichomea taka na kumalizia jengo la upasuaji 'theater'.
No comments:
Write comments