Watalamu wakaguzi wa nyama halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru wamelazimika kuzuia ulaji wa nyama ya ng'ombe aliyechinjwa na kupimwa na kugundulika kuwa na dalili za ugonjwa uliosababisha ini kushindwa kufanya kazi.
Daktari wa Mifugo halmashauri ya Arusha Dkt. Linus Prosper amesema kuwa ng'ombe huyo alichinjwa katika machinjio ya Sanawari na baadaye kupimwa nyama yake na hatimaye kuzikwa mara baada ya madaktari hao wa mifugo kugundua nyama hiyo hafai kwa matumizi ya binadamu.
Dkt. Linus amesema kuwa wamelazimika kufukia nyama ya ng'ombe huyo baada ya kuthibitika kuwa na ugonjwa uliosababisa ini kushindwa kufanya kazi na amefafanua kwa lugha ya kitaalamu kuwa ni icterus, haemorrhage, multiple hepatic abscesses.
"Tumelazimika kufukia nyama hiyo kutokana na kuwa nyama hiyo haikuwa salama kwa mlaji, ukiangalia maini yote yalikuwa na majipu, nyama yote ilikuwa ya rangi ya njano na pia imetapakaa damu " amefafanua Dkt.Linus.
Hata hivyo Dkt. Linus amewataka wafugaji kuacha tabia ya kuchinja ng'ombe wenye magonjwa au walio kwenye matibabu kwani wana madhara kwa afya na kuwataka wananchi kuwa na tahadhari kwa kuacha kula nyama zilizochinjwa nyumbani bila kupitia kwenye machinjio rasmi.
"Huyu ng'ombe tumegundua tatizo hilo kwa kuwa aliletwa machinjoni lakini angechinjiwa nyumbani watu wangemla jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mlaji"amesema
Aidha amewatoa hofu wananchi kuwa ugonjwa huo sio wa mlipuko ni magonjwa ya kawaida kwa ng'ombe.
No comments:
Write comments