Mkuu wa mkoa wa Manyara mheshimiwa Alexander Mnyeti aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Arumeru amepata fursa ya kuagana na watumishi wa halmashauri ya Arusha kwa kukutana na watumishi wa makao makuu kwenye hafla fupi ialiyofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano halmashauri ya Arusha.
Mheshimiwa Mnyeti amefanikiwa kufanyakazi katika halmashuri hiyo kwa takribani miaka miwili na miezi michache kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Manyara mwishoni mwa mwezi Oktoba 2017.
Mnyeti amewaaga watumishi wa halmashuri ya Arusha kwa kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa upendo na ushirikiano huku wakiweka mbele uzalendo kwa lengo la kuwatumikia wananchi wa halmashauri hiyo ili kuleta maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Aidha mkuu wa mkoa huyo hakusita kuwashukuru na kumwaga sifa nyingi kwa watumishi hao kwa kusema kuwa anawapongeza kwa uchapakazi wao usio kifani licha ya changamoto nyingi zilizopo na kuongeza kuwa ushirikiano aliupata kutoka kwao uendelee na usiishie kwake tu.
"Ninashukuru kwa uchapakazi wenu na ushirikiano mlioninyesha natamani uchapa kazi huu uendelee hata kwa mkuu wa wilaya atakayekuja, zaidi tusameheane pale tulipopishana kwa namna yoyote ile, hiyo ilikuwa ni katika kuwajibika na nina wakaribisha sana mkoani Manyara" amesisitiza Mnyeti
Akizungumza kwa niaba ya watumishi hao katibu Tawala wa wilaya ya Arumeru Timotheo Mzava ametoa pongezi kwa mheshimiwa Mnyeti kwa kuaminiwa na mheshimiwa Rais na kuteuliwa mkuu wa mkoa na kumtaka kwenda kuwatumikia wananchi wa Manyara licha ya kwamba juhudi zake bado zinahitajika wilayani Arumeru.
Aidha Katibu Tawala huyo ameahidi kuendelea kutekeleza shughuli zote ambazo zilikuwa kwenye mipango na kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kama yalivypangwa.
"Nikuhakikishie mheshimiwa Mkuu wa mkoa wa Manyara shughuli zote tulizokuwa tumepanga kufanyika tutazikamilisha kwa nguvu zote na kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi wetu" amesema Katibu Tawala.
Hata hivyo watumishi wa halmashauri ya Arusha licha ya kusikitishwa kuondoka kwa mkuu wao wa wilaya ambaye walimwita Jembe lakini pia wamempongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kipindi kifupi pamoja na kutambua umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii.
Mweka Hazina wa Halmashauri ya Arusha ndugu Munguabela Kakulima amesema kuwa tunasikitika kuondoka kwake lakini pia tunampongeza na kuahidi kuendelea kuenzi uchapakazi wake.
"Tunampongeza na kumtakia kila la heri katika utumishi wake kama mkuu wa mkoa zaidi uteuzi wake ni funzo kwetu la uwajibikaji katika kazi na kulitumikia taifa" amesema
Naye Afisa Vijana halmashauri ya Arusha Ahadi Mlai amempongeza mkuu huyo wa wilaya na kuongeza kuwa amekuwa mchapakazi na kiongozi mwenye kuhakikisha anawaongoza wanachapa kazi bila uzembe.
"Kwa kipindi chote alichokuwa Arumeru ameonyesha mfano wa kiongozi mchapa kazi kwa watumishi kwa kuwafanya watumishi kuwajibika kwa kadiri ya uwezo wao kwa lengo la kuwatumikia wananchi"amesema Afisa Vijana
Baada ya uteuri wa mheshimiwa Mnyeti, Wilaya ya Arumeru inakaimiwa na Mkuu wa wilaya ya Longido mheshimiwa Daniel Chongolo baada ya kuteuliwa mkoa wa Arusha mheshimiwa Mrisho Gambo kukaimu nafasi hiyo.
PICHA ZA MATUKIO YA HAFLA HIYO
.
No comments:
Write comments