Wananchi wametakiwa kufahamu kuwa rasilimali maji ni mali ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inamilikiwa na mheshimiwa Rais na si mali ya mtu yoyote wala wananchi wa eneo yanapopatikana maji.
Rai hiyo imetolewa na Fundi Sanifu halmashauri ya Arusha Peter Maina wakati wa mkutano kati ya timu ya watalamu wasimamizi wa mradi wa maji wa vijiji vitano maarufu kama mradi wa maji wa WaterAid na wajumbe wa serikali ya kijiji cha Olkokola kata ya Lemanyata.
Maina amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya wajumbe hao kulalamikia na kuhoji kwa nini mradi mpya wa maji utumie chanzo cha maji cha Tiasilele, chanzo ambacho kinatumika kwa wakazi wa Olkokola na Mwandeti na kuhofia kuathiri mradi wao wa zamani.
Maina ameongeza kuwa maji ni rasilimali ya umma na mtu yoyote anayeishi Tanzania ana haki ya kutumia kwa kiasi kinachotosheleza hivyo chanzo cha maji cha Tiasilele si cha mali ya Mwandeti wala Lemanyata ni ya watanzania wote.
Aidha ameweka wazi sheria ya utunzaji wa rasilimali maji sheria namba 11 ya mwaka 2009 inabainisha kuwa maji ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yanasimamiwa chini ofisi za Mabonde na kuongeza
"Maji yale ya Tiasilele ni mali ya serikali chini ya usimamizi wa Bonde la Pa ngani na wataalamu wamepima kiasi kile cha maji na kuona kitatosheleza hivyo hakuna athari zozote zitakazotokea na kuathiri miradi mingine ya maji na badala yake miradi hiyo itaiboreshwa" amesema Maina
Hata hivyo watalamu hao walielezea kuwa mradi huo wa maji utagharamiwa kwa asilimia mia moja hivyo wananchi wanatakiwa kushiriki kwa hali na mali kwenye mradi huo kwa kuruhusu maeneo yao kupitisha miundo mbinu ya maji kama mabomba.
Afisa Ardhi Mteule halmashauri ya Arusha amefafanua kuwa ushiriki wa wananchi katika mradi ni kutoa maeneo ambayo miundo mbinu ya maji itapitishwa licha ya kwamba ni takwa la kisheria kulipa fidia ya ardhi hivyo wananchi wa Olkokola wanapaswa kujitoa kwa hilo.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Arusha ameweka wazi kuwa ushiriki wa wananchi katika mradi huo wa maji ni pamoja na kukubali mradi kuwa ni mali yao, kutunza mazingira ya vyanzo vya maji, kusimamia na kuendeleza mradi huo kwa kulipia huduma za maji pamoja na kutoa maeneo kwa ajili ya kupitisha miundo mbinu ya maji bila kulipwa fidia yoyote.
Licha ya maswali na majibu iliyoambatana na mijadala mirefu wajumbe hao wa serikali ya kijiji walikubaliana kushiriki kwa hali na mali katika kwa kutoa maeneo pamoja na kukubali kulipia maji.
Mzee Joseph Lowasare mjumbe wa serikali ya kijiji amesema kuwa kuna umuhimu wa wananchi fahamu hali imebadilika ili kupata huduma ni lazima kulipia bila kulipia huduma nyingi zinakufa.
" Serikali iliwahi kuletewa matreka ya kuwakopesha wakulima, watu wakajazana ujinga wakakataa yakapekekwa Meru wenzetu wakatajirika nayo, nashauri wenzangu tusikubali tukprudia ujinga ule, tupokee mradi tukubali kulipia kwa maendeleo yetu na vizazi vyetu" amesisitiza Mzee Lowasari.
PICHA ZA MKUTANO WA VIONGOZI WA SERIKALI YA KIJIJI CHA OLKOKOLA KATA YA LEMANYATA
No comments:
Write comments