Tuesday, October 10, 2017

Watendaji watakiwa kufikia malengo kwa kukamilisha ujenzi wa vituo vya Afya

Mgeni Rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Maimuna Tarishi akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Watendaji wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma. Kikao hicho kilihusu kupeana uelewa wa ujenzi na ukarabati wa vituo vya Afya 172 ambavyo imeagizwa vikamilike kabla ya Desemba 30, 2017.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Dkt. Zainab Chaula akitoa neno wakati akimkaribisha Katibu Mkuu OR TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe kutoa neno la ukaribisho kwa mgeni Rasmi Bi. Maimuna Tarishi ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kikao kazi hicho kilihusu kupeana uelewa wa ujenzi na ukarabati wa vituo vya Afya 172

Katibu Mkuu OR TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe akitoa neno la ukaribisho kwa mgeni Rasmi Bi. Maimuna Tarishi ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Katibu Mkuu Mhandisi Iyombe pia aliwataka Watendaji wote wawajibike katika maeneo yao ya kazi na kwamba Mtendaji atakayekiuka majukumu yake basi atawajibishwa kwa mujibu wa taratibu.

Baadhi ya Washiriki kutoka OR TAMISEMI, Wizra za Kisekta, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wadau wengine wakiwa katika kikao kazi kuhusu kupeana uelewa wa ujenzi na ukarabati wa vituo vya Afya 172, kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Hazina uliopo mjini Dodoma.

Mstahiki Meya wa Shinyanga Mhe.Gulam Hafidhi Mukadamu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) akitoa neno kwa Washiriki wakati wa Ufungaji wa kikao kazi mjini Dodoma kuhusu kupeana uelewa wa ujenzi na ukarabati wa vituo vya Afya 172. Mstahiki Meya Mukadamu aliwataka Watendaji wote kufanya kazi kwa bidii ili kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kama ilivyoagizwa katika Serikali ya Awamu ya tano

Na Asila Twaha

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Maimuna Tarishi amefungua kikao kazi cha Viongozi na Watendaji wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa mjini Dodoma ili kupeana uelewa wa pamoja kuhusu ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya nchini.

Akifungua kikao hicho Bi. Maimuna Tarishi amesema Serikali kupitia, “Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu itahakikisha inasimamia majukumu hayo kwa ufanisi na kupeana majukumu katika eneo la afya lengo likiwa ni ukarabati wa vituo vya afya 556 na kwa mwaka huu ni vituo 172”

Amesema ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto Serikali ya awamu ya tano inafanya jitihada kwa kutoa fedha za kuboresha na kukarabati vituo vya afya ili wananchi waweze kupata huduma bora ya afya kwa ustawi wa Taifa.

Katika hatua nyingine Bi. Tarishi akitoa hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI amewaagiza Watendaji wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia ukarabati unaoendana na thamani halisi ya fedha, matumizi ya Force account ili kupunguza gharama za ujenzi na ukarabati, kukamilisha ujenzi wa vituo vya awali ifikapo Desemba 30, 2017 na Makatibu Tawala wa Mikoa kutoa taarifa kila tarehe 5 ya kila mwezi kwenda Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe amesisitiza kuwa Sekta ya Afya bado inachangamoto nyingi kuanzia majengo na huduma itolewayo hivyo ni lazima Viongozi wawajibike katika maeneo yao ya kazi na kwamba Mtendaji atakayekiuka majukumu yake basi atawajibishwa kwa mujibu wa taratibu.

Mhandisi Iyombe ameipongeza Halmashauri ya Kakonko kwa kufanya vizuri katika kutekeleza majukumu yao hasa katika sekta hiyo muhimu ya afya chini.

Naye Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais –TAMISEMI Dkt. Zainab Chaula wakati akiwasilisha mada amesema kuwa ametembelea vituo vingi vya afya nchini na kubaini changamoto nyingi lakini pia ni kutowajibika kwa Viongozi kwa pamoja na kutokuwa wawazi na kuweka vipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu ya afya. “Ofisi ya Rais –TAMISEMI imejipanga na kufanya uboreshaji wa miundombinu katika vituo vyetu, kudhibiti makusanyo ya mapato yatokanayo na vituo vyetu, uboreshaji wa takwimu kwa kutumia mfumo (GoTHOMIS) na upelekaji wa fedha moja kwa moja katika vituo vyetu vya afya”

Dkt. Chaula amesema, Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuratibu utekelezaji wa Program za Maendeleo ya Wizara za Kisekta ili kuboresha huduma za afya nchini.

Aidha, amewataja baadhi ya Wadau walioshiriki katika kuchangia sekta ya afya nchini kuwa ni pamoja na Benki ya Dunia, Canada HBF, Programu ya Umoja wa Mataifa (UNFPA) na Ubalozi wa Dernmark. Amesisitiza Watendaji wote kufuata utaratibu wa matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa katika kuboresha huduma za afya nchini.

Sekta ya afya ni moja ya Sekta muhimu nchini ambapo Serikali ya Awamu ya tano hali ikitekeleza Ilani ya Chama Tawala imeendelea kuwekeza fedha katika vituo vya afya ili kuhakikisha watanzania wanakuwa na afya bora kuelekea Tanzania ya Viwanda

 

Source:  Tamisemi Blogu

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo
Loading...