Tuesday, October 31, 2017

Wakazi wa Halmashauri ya Arusha kupata maji kwa asilimia 80%


Tatizo la maji kwa wakazi wa halmashauri ya Arusha linategemewa kupungua ifikapo mwaka 2018/19 kwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi  hadi kufikia zaidi ya 80% kutoka asilimia 54.2 za sasa.

Hayo yamethibitishwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack  Kamwele alipokutana na wataalam wasimamizi wa mradi wa maji wa vijiji vitano  halmashauri ya Arusha maarufu kama mradi wa WaterAid walipokutana  kwenye hotel ya Mount Meru jijini Arusha na kuthibitisha kuwa mkakati wa serikali ni kuhakikisha maji yanapatikana kwa zaidi ya asilimia 90% .

Waziri Kamwele amethibitisha kutekeleza ahadi yake ya shilingi bilioni 2.3 aliyoitoa mwezi Februari,  2017 akiwa Naibu Waziri wa Maji aliahidi kutoa kiasi hicho cha fedha kwa lengo la kupanua mradi wa maji wa  OLMULO unaohudumia wakazi wa kata za Oljoro na Laroi halmashauri ya Arusha.

Waziri Kamwele amesema kuwa fedha hizo zitatolewa ndani ya mwaka huu wa fedha ili huduma ya maji ipatikane  umbali usiozidi mita 400 kwa kila mwananchi ifikapo mwaka 2020.

Hata hivyo Waziri Kamwele ameahidi kutoa fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili kuendeleza chanzo cha maji cha Emutoto kilichogundulika wakati wa upembuzi yakinifu wa mradi wa maji wa vijiji vitano mradi unaotekelezwa na shirika la kimataifa la WaterAid.

Waziri huyo amefikia uamuzio huo wenye lengo la kuongezea nguvu za upatikanaji  wa huduma ya maji kwenye kijiji cha Ilkuroliti na baadhi ya maeneo ya kata ya Oldonyosambu ambayo licha ya kuwa na uhaba wa maji wanakabiliwa na tatizo la Floraidi iliyozidi kwenye maji ya eneo hilo.

Mhandisi wa Maji halmashauri ya Arusha Mhandisi Joyce Bahati amesema kuwa fedha hizo zitasaidi kuongeza nguvu kwenye mradi wa vijiji vitano ambao tayari upembuzi yakinifu umekwishafanyika na kuwa ni njia rahisi ya kuongeza matawi zaidi.

Ameongeza kuwa mradi wa vijiji vitano ulikuwa uwafikie watu elfu hamsini lakini endapo mradi utaongezeka utaongeza watu zaidi ya elfu tano wa vijiji vya Ilkuroti na baadhi ya maeneo ya Oldonyosambu.

Aidha Mhandisi Bahati amesema kuwa kuendeleza chanzo cha Emutoto kitasababisha  urahisi wa kuendeleza matawi kwenye vijiji ambavya havina maji kwa kuelekea ukanda wa Oldonyosambu zaidi.

Mradi wa maji wa vijiji vitano umefadhiliwa na shirika la Maendeleo la Uingereza DFID na kutekelezwa na shirika la WaterAid unategemea kuhudumia watu elfu hamsini kwenye vijiji vya Lengijave na Olkokola na vitongoji vya Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 na kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja. 







No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo