Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbas amethibitisha kuwa serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 530 kwa ajili ya kupandisha madaraja wafanyakazi kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk Hassan Abbas alisema kwa sasa Serikali imemaliza mchakato wa awali wa kusafisha watendaji hewa kwenye mfumo na wale ambao wataonekana kuwa ni halali mchakato wa kupandisha madaraja utaanza.
Alisema kwa sasa Serikali inatekeleza na kufanyia kazi agizo la kupandisha wafanyakazi madaraja na katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha Serikali imetenga Shilingi bilioni 487.7 kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi baada ya kuanza kwa mfumo mpya na kuondoa wafanyakazi wenye utata.
“Mchakato wa kupandisha madaraja unaendelea na wengine ambao hakuna mchakato mrefu kuwapandisha madaraja wamekwishapandishwa na wamelipwa na tayari katika robo hii Shilingi milioni 531 zimeshalipwa kwa waliopanda katika ngazi zisizo na utata,” alisema.
Dk Abbas alisema Serikali imetenga Shilingi bilioni 35.2 kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi huku Shilingi bilioni 70.4 zikilipwa kwa ajili ya madai ya wafanyakazi sehemu kubwa ikiwa ni madai yasiyo ya mishahara kwa mwaka wa fedha 2016/17 katika robo hii ya kwanza.
Awali mkurugenzi huyo alikanusha taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) kuhusu kauli ya Rais John Magufuli kutopandisha mishahara kwa wafanyakazi na Dk Abbas alisema kauli hiyo ililenga posho za madiwani na si wafanyakazi wote.
“Si kweli kuwa kauli ilijikita kwa wafanyakazi wa umma bali ni madiwani waliotaka kuongezewa posho kutoka Shilingi 350,000 hadi shilingi 800,000 na si wafanyakazi na sisi kama Serikali tutawachukulia hatua walioeneza taarifa hii ya uongo,” alisema.
No comments:
Write comments