Friday, September 8, 2017

Mongella: Wanaume wengi hawajui kutongoza


Mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati wa zamani wa haki za wanawake na watoto, Balozi Getrude Mongella amesema vitendo vya ubakaji kwa watoto vinaongezeka kwa sababu baadhi ya wanaume hawajui ‘kutongoza’.

Akizungumza na gazeti hili jana wakati wa Tamasha la Jinsia linaloendelea kwenye viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), balozi Mongella alisema isingekuwa hivyo matukio hayo ya kikatili kwa watoto yangepungua kwa kiwango kikubwa.

“Hii hali inaumiza, kibaya zaidi wanaoumia ni watoto wetu lakini haya yote ni kwa sababu baadhi yao wameshindwa kutongoza,” alisema. Balozi Mongella alisema ukatili wa kijinsia unaweza kupungua iwapo jamii itakubali kubadili tabia na kuwalinda watoto, ili watimize ndoto zao kimaisha.

Kwenye kijiwe cha simulizi ya maisha yake, Balozi Mongella alisema mafanikio yake kisiasa yanatokana na namna alivyolindwa tangu udogo wake hadi sasa, jambo ambalo lazima watoto wafanyiwe ili kutimiza ndoto za maisha yao.

Aliwataka wanaharakati kuweka mkakati wa kufuatilia mambo wanayoyapanga na kuyafikisha kwa viongozi wa Serikali, ili yafanyiwe kazi badala ya kurudia yaleyale kila siku.

“Tuache kuparamia wenye nafasi zao, tuandae mipango yetu na tujue namna ya kuwafikishia ili wayatatue. Tushinikize kwa lugha nzuri,” alisema. Aliendelea kuwa lazima wanawake wazungumze namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia, zikiwamo mimba za utotoni ili kutengeneza jamii iliyo sawa.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo