Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema matukio ya kutekwa watoto katika jiji la Arusha yameipa wakati mgumu kamati ya ulinzi na usalama mkoa na kujipanga kuhakikisha matukio hayo yanadhibitiwa.
Akizungumza katika msiba wa Mtoto Maureen David Njau (6) aliyeuawa na mtuhumiwa Samson Petro (18) mkazi wa mkoa wa Geita Septemba akiwa mwenzake Ikram Salim, Gambo amesema ni lazima polisi isambaratishe mtandao wote wa watekaji.
Gambo amesema tukio la kutekwa watoto bado kwake ni mtihani mkubwa pamoja na kamati ya usalama mkoa na imefika wakati kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake katika kuimarisha ulinzi na usalama katika Jiji la Arusha.
"Tunaomba wananchi watoe ushirikiano wa kutosha katika kuwafichua wahalifu wa mtandao huo kwani wapo mtaani na mnaishi nao na wengi wao mnawafahamu kwa hiyo naomba ukiona unaishi na mtu ambaye humwelewi mienendo yake uripoti katika vyombo vya ulinzi na usalama ili aweze kufuatiliwa. "amesema Gambo.
Aidha kutokana na tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema watajenga vituo viwili vya polisi katika Kata ya Olasiti na Muriet kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili iweze kupunguza uhalifu katika maeneo hayo.
Gambo amesema kuwa, bahati nzuri kupatikana kwa mtuhumiwa huyo wa Geita ni juhudi za Jeshi la polisi na kufuatia matukio hayo aliyowafanyia watoto hao naye pia Mungu ameweza kumpatia hicho alichowafanyia wenzake.
Gambo , ametoa milioni 2 za rambirambi katika msiba huo ambapo milioni moja atawapatia wazazi wa Maureen huku nyingine wakipatiwa wazazi wa Ikram Hassan.
Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Viola Lazaro kata hiyo ina wageni wengi, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anakuwa mlinzi wa mwenzake kwani kijana huyo aliyefanya uhalifu huo alikuwa anaishi na watu na kama wangeripoti mapema hatua zingechukuliwa mapema.
Viola amewataka polisi kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja katika kuendelea kuufichua mtandao huo ili kuwezesha kukomesha matukio hayo yasiendelee kushika kasi kwa mkoa wa Arusha na hata Tanzania kwa ujumla.
Naye diwani wa Kata ya olasiti, Alex Martin amesema kuwa, hali ya uhalifu katika mkoa wa Arusha hivi sasa umeshika kasi Sana ambapo unasababishwa na Watu waovu ambao tunaishi nao katika maeneo yetu na hata wengine wanafahamika lakini hawafichuliwi na matokeo yake ndio hayo.
"Zamani kulikuwa na matukio ya kupotea ng'ombe na baadaye zinapatikana ila kwa sasa hivi inakuwaje binadamu anapotea na anakutwa maiti ni kitu cha kusikitisha tunaomba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake katika kufichua uhalifu miongoni mwetu. "amesema Alex.
Naye wakili wa kujitegemea, Albert Msando aliyetoa milioni moja za rambirambi amesema ni wakati sasa wa kuungana pamoja na kuanzisha kampeni ya kuwalinda watoto wetu kutokana na kukumbwa na matukio mbalimbali ya kikatili yakiwemo ya ulawiti, ubakaji na mauaji vitendo vinavyofanywa na watu wasiokuwa na hofu yoyote.
No comments:
Write comments