Tuesday, September 19, 2017

Kamanda Fortunatus Musilimu ametangaza kiama kwa madereva wasiotaka kutii Sheria za barabarani.


Dar es Salaam. Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani, Kamanda Fortunatus Musilimu ametangaza kiama kwa madereva wasiotaka kutii Sheria za barabarani.

Amesema hayo leo wakati wa Shindano la Uchoraji wa Picha za Kampeni ya Usalama barabarani kwa wanafunzi wa Mkoa wa Dar es Salaam lilofanyika katika Shule ya Msingi Diamond na kuratibiwa na Kampuni ya Puma Energy pamoja na Amend.

Amesema katika kutekeleza hilo, hatojali Cheo, Sura au Jinsia ya mtu yoyote ambaye atakiuka Sheria zilizowekwa.

"Nitapambana na madereva wasiofuata sheria kwa nguvu zangu zote,"amesema na kuongeza:

" Rais Magufuli anatumia maneno mawili tu kwa watu wasiotaka kulipia ankara za umeme,anasema "KA-TA", sasa mimi natumia maneno matatu tu "KA-MA-TA, ",amesema

Amesema Kikosi chake kimejipanga katika kuimarisha usalama kwa wanafunzi wote wakati wanapozitumia barabara wakati wa kwenda Shule na kurudi majumbani.

Ameipongeza Kampuni ya Puma kwa kuendesha Kampeni ya usalama barabarani kupitia uchoraji na kwamba inawajengea uwezo wanafunzi kwa kupata elimu na kujua namna ya kujikinga na ajali.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Puma Energy hapa nchini,Phillipe Corsaletti amesema wameendelea kutoa elimu kwa wanafunzi ikiwa ni mkakati wa kupunguza vifo vitokanavyo na ajali kwa manufaa ya Kizazi kijacho.

Amesema hadi sasa elimu hiyo imezifikia shule zaidi ya 47 na kuwafikia wanafunzi zaidi ya 60,000 huku wakilenga kutanua wigo kuzifikia Shule zote nchini.

"Watoto wa shule ni hazina kwa Taifa, na suala la usalama wao linabaki kuwa moja ya agenda kwa kampuni yetu, "amesema

Naye, Mkurugenzi msaidizi wa Kampuni ya Amend,Tom Bishop amesema kila mwaka watu zaidi ya 1.2 Milioni hupoteza maisha huku zaidi ya 50Milioni wakijeruhiwa duniani.

Amesema hali inaonyesha Tanzania ajali zimekuwa zikipungua kutokana na jitihada za uelimishaji zinazofanywa na wadau mbalimbali.

Katika Shindano hilo lililoshirikisha Wanafunzi kutoka Shule zaidi ya 12,Mwanafunzi kutoka Shule ya msingi ya Amani,Nasri Meena (darasa la tano) ameibuka mshindi baada ya kuchora picha kwa ustadi mkubwa.

Mshindi amekabidhiwa hundi ya Sh 2 milioni na kikombe, begi na madaftari kutoka Kampuni ya Puma Energy.

Mwananchi:

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo