Mkuu wa Mkoa wa Arusha mheshimiwa Mrisho Gambo ameweka mikakati ya kutatua kero zilizowasilishwa na wananchi wa kata ya Kisongo na vijiji vyake alipotembelea Kituo cha Afya Engorora na kuzungumza na wananchi wa kata ya Kisongo ambao walipewa fursa ya kutoa kero zinazowakabili.
Licha ya wananchi kuelezea kero zao wananchi hao walimuelezea mkuu wa mkoa Gambo kuwa wananchi hao wanakabiliwa na tatizo la maji, miundo mbinu mibovu ya barabara, umeme pamoja na kero binafsi za wananchi wa kata ya Kisongo.
Baada ya kusikiliza kero hizo mkuu wa mkoa wa Arusha ametoa fursa kwa wataalamu wa sekta zilizolalamikiwa kujibu kero hizo ambapo Meneja wa TANESCO Gasper Msigwa amethibitisha kuwa kijiji cha Engorora kipo kwenye mpango wa REA awamu ya tatu.
Aidha ameagiza Idara ya Ardhi kushughulikia malalamiko ya wananchi waliochanga fedha kwa ajili ya kupimiwa na kupewa hati Miliki za Kimila katika maeneo yao lakini walipimiwa bila kupewa hati hizo.
Mkuu wa mkoa huyo ametoa agizo hilo baada ya Afisa Ardhi Mteule Rehema Jato kufafanua kuwa utaratibu huo wa wananchi kupewa hati hizo za Kimila ulifanywa na mkuu wa Wilaya aliyekuwepo mwaka 2013 kwa kuwapatia mafunzo vijana kutoka kwenye vijiji vyao na kuwaandalia hati jambo ambalo Ofisi ya Ardhi halmashauri haikushirikishwa.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Engorora Mwenyekiti wa Kijiji cha Engorora Justine Laizer amemuomba mkuu wa mkoa kumchangia ujenzi wa nyumba ya watumishi yenye sehemu mbili 2 in 1 ambapo alimuhakikishia mkuu wa mkoa endapo atamchangia mifuko 100 ya saruji na mabati 100 ndani ya miezi michache takuwa amemaliza ujenzi wa nyumba hizo wa watumishi wa Afya.
Katika hali ya isiyokuwa ya kawaida mkuu wa mkoa amekubali ombo hilo na kuahidi kutoa mifuko 100 ya saruji na mabati 100 kwa sharti la kuhakikisha nyumba hiyo inakamilika kwa wakati kama walivyo ahidi.
Hata hivyo mkuu wa mkoa aliongeza kutoa mifuko mingine 20 ya saruji kwa ajili ya kujenga kivuko kwenye barabara inayounganisha kijiji cha Ngorbob na Kijiji cha Ematasia na kuwataka wananchi hao kuchangishana kujenga kivuko hicho kwa kutumia mitambo inayomilikiwa na halmashauri ya Arusha ili kuondokana na adha hiyo.
Wananchi wa Kiji cha Engorora wamzawadia mbuzi mkuu wa mkoa wa Arusha na kumuomba kuwa Mlezi wa Kituo chao cha Afya na mbuzi huyo ni ishara ya upendo.
Picha za matukio yaliyojiri katika Kituo cha Afya Engorora
No comments:
Write comments