Wednesday, September 13, 2017
Mkuu wa Mkoa Gambo aahidi kumpa pikipiki kijana Shedrack wa kata ya Ilkiding'a
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ameahidi kumpa pikipiki kijana Shedrack Piniel mkazi wa kata ya Ilkiding'a wakati akipokea kero za wananchi wa Ilkiding'a kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye shule ya sekondari ya Ilkiding'a siku ya tatu ya ziara yake katika halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru.
Mheshimiwa Gambo amefikia uamuzi huo baada ya kijana Shedrack kulalamika huku akitoa machozi mbele ya mkuu wa mkoa huyo kuwa yeye ni yatima amelelewa na bibi yake baada ya wazazi wake kufariki akiwa mdogo na aliandikwa jina ili aingizwe kwenye mpango wa TASAF lakini jina lake halikurudi.
"Mimi ni yatima jina langu liliandikwa TASAF lakini mpaka leo sipati fedha na wengine wanapata na zaidi watu wananisema nina UKIMWI tangu wazazi wangu wafe, kwa nini waninyanyapae" alihoji Shedrack huku akilia
"Hata mimi nimesikia uchungu sana kwa maneno ya huyu bwana nitakupa pikipiki bure ili ikusaidie kukabiliana na maisha wala usiwe na wasiwasi" amesisitiza Gambo.
Hata hivyo mkuu wa mkoa amefanikiwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo ombi la kutaka barabara ya lami na kuwathibitishia wananchi hao kuwa barabara ya Mianzini-Ilkiding'a -Sambasha itajengwa kwa kiwango cha lami umbali wa Kilomita 1 kwa a awamu ya kwanza ambayo tayari mkandarasi amepatikana.
Aidha amewataka wananchi hao kuacha malumbano badala yake wakae pamoja na kujadili namna ya kuchangia maendeleo ya eneo lao kwa kuwa nchi yetu itajengwa na watanzania wenyewe, zaidi ametaka elimu itolewe kwa vijana kwa ajili ya kuunda vikundi ili wapatiwe mikopoinayotolewa na halmashauri kupitia asilimia 10% za mapato ya ndani.
Mkuu wa mkoa huyo anaendelea na ziara ya kikazi ya siku tano katika halmashauri ya Arusha kwa kutembelea na kukagua shughuli za utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kufanya mikutano ya hadhara ambayo anatoa fursa kwa wananchi kutoa kero, changamoto na ushauri katika maeneo yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Write comments