Sunday, August 13, 2017

Waziri wa Ardhi aagiza kutolewa haraka vibali vya ujenzi


Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaagiza viongozi wa halmashauri na majiji nchini kuachana na urasimu wa kutoa vibali vya ujenzi jambo linaosababisha kuwepo kwa ujenzi holela badala yake kuharakisha utoaji wa vibali vya ujenzi.

Lukuvi ameyasema  hayo alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa nyumba  kumi za  mfano za mradi wa mji wa kisasa wa  Safari City  zilizopo eneo la Mateves jijini Arusha sambamba  na kutoa hati miliki kwa wanunuzi 100 wa kwanza wa viwanja zinazotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Amesema kuwa kumekuwepo urasimu  unaosababisha ucheleweshaji mkubwa wa vibali vya ujenzi unaosababishwa na wahusika wenyewe na hivyo kuchangia  wananchi hao kujenga kiholela kutokana na kuchoka kusubiri  kwa muda mrefu.

Kufuatia hali hiyo Waziri Lukuvi amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kufanya ukaguzi wa mafaili ya vibali vya ujenzi ili kubaini idadi ya watu walioomba vibali na hawajapatiwa vibali vyao mpaka sasa.

"Unajua idadi kubwa ya wananchi wanaojenga kiholela siyo kwamba wamevunja sheria bali wanafanya hivyo kwa ajili ya ucheleweshaji wa vibali  na msiwalazimishe wananchi kusubiri kwa muda mrefu sana bila kuwapatia majibu yanayoeleweka kwani nyie wenyewe ndio mtakuwa mnachangia ujenzi holela. "amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema kuwa, ni aibu na fedheha wananchi kukaa katika maeneo holela kwani wanachangia kuharibu madhari ya Jiji ,na hivyo kuwataka kujenga maeneo yaliyopimwa.

Naye  Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nyumba la taifa NHC ndugu Nehemia Mchechu amesema kuwa mradi huo wa kitovu cha mji wa kisasa wa safari city jijini hapa una ukubwa wa hekari 559.4 na ni sehemu ya miji iliyopangiliwa kitaalamu na kwa kuzingatia sheria za mipango miji.

"Mradi huu ulibuniwa na shirika la nyumba kwa lengo la kupunguza uhaba wa makazi kwenye jiji la Arusha mbapo tumetenga maeneo kwa ajili ya waendelezaji kujenga sehemu za biashara,burudani ,utalii,hospitali, elimu,huduma za kijamii kama vile polisi,na zimamoto lakini pia yapo maeneo ya wazi kwa ajili ya michezo na mapumziko" amesema Msechu.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo