
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan amesewatahadharisha watanzania kuwa serikali haitatoa chakula wilaya zitakazokuwa na njaa.
Mama Samia ameyasema hayo wakati akihutubia taifa katika sherehe za kilele cha maonyesho ya wakulima 'Nane Nane' yaliyofanyika kitaifa katika eneo la Ngongo mkoani Lindi, na kusema kuwa serikali itabeba jukumu la kulisha chakula kwa zile wilaya ambazo zitapata maafa ya kiasili na sio kwa uzembe na uvivu.
Aidha Makamu wa Rais amewataka wakuu wa wilaya kuhakikisha wananchi katika wilaya zao wanazalisha chakula cha kutosha kwa kuwa serikali haitabeba jukumu la kulisha wilaya zitakazokumbwa na njaa.
“Uhakika wa upatakanaji wa chakula unaanza nyumbani kwako, jinsi unavyovuna na kujitengea chakula,tuwaambie wakuu wa wilaya hatutalisha wilaya inayolia njaa kwa uzembe hivyo niwatake wakuu wa kuhakikisha chakula cha kutosheleza kinapatikana katika wilaya zenu" amesema mama Samia Suluhu
Aidha Makamu wa Rais amefafanua kuwa serikali itachukua jukumu la kulisha chakula kwenye wilaya ambazo zimepata maafa peke yake, tukifanya hivyo tutaipunguzia serikali mzigo mkubwa wa kulisha watu.
Hata hivyo mama Samia amewataka Watanzania wote kuendelea kuwa na mshikamano na kufanya uzalishaji wa chakula kwa kiasi kikubwa ili nchi ipunguze kuomba misaada kutoka nje.
“Tunaposema Watazania tushikane na tufanye kazi kwani hatuna wajomba wa kutusaidia, naomba sana tushikamane tufanye kazi tuzalishe kwa wingi, tufike pale tunapotaka kwenda”, amesisitiza Mama Samia Suluhu.

No comments:
Write comments