Kamishna mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga alisema jana kuwa Watanzania hao walikamatwa mpakani mwa nchi ya Msumbiji na Swaziland wakiwa na mzigo huo.
“Kinachofanyika sasa ni kwamba tunashirikiana na nchi ya Swaziland ili kujua watanzania hao wanashirikiana na akina nani na mtandao wao kwa ujumla,” alisema Sianga.
Taarifa zinadai kuwa Watanzania hao walikamatwa juzi na maofisa wa polisi wa Swaziland wakiwa na dawa za kulevya zilizofichwa ndani ya buti la gari.
Maofisa hao baada ya kufanya upekuzi walibaini mifuko ya plastiki miwili ya rangi nyeusi.
Inadaiwa kuwa kila pakiti yenye dawa hizo iliwekwa pilipili ili kuzuia mbwa waliokuwa wanatumiwa kupekuwa wasibaini harufu za dawa hizo za kulevya.
“Kwa kuwa sasa hivi tumewabana wafanyabiashara hao haramu wa dawa za kulevya, wameamua kukimbilia Msumbiji kwa ajili ya kufanya biashara hiyo. Soko kuu lipo Afrika Kusini na mara nyingi wanawawekea dhamana (bond) vijana kusafirisha na wanapofanikiwa wanalipwa fedha zao,” alisema.
Alifafanua kuwa kutokana na kushamiri kwa wafanyabiashara hao, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanyiwa marekebisho ya sheria mpya kifungu cha 15 ikiwamo kuongezea kosa la kuweka mtu rehani kwa minajili ya kufanikisha biashara hiyo, huku adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.
Kamishna wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Edwin Kakolaki alisema makosa mengine chini ya kifungo hicho ni kusafirisha dawa za kulevya na kuchepusha, kusafirisha isivyo halali kemikali bashirifu.
Kakolaki aliongeza kwamba marekebisho mengine ya sheria hiyo ni kuipa uwezo mamlaka hiyo kushughulikia makosa mengine yenye uhusiano wa moja kwa moja na biashara na matumizi ya dawa za kulevya kifungu cha 4(2)(f).
Zaidi ya hilo pia alisema kwamba marekebisho mengine yanampa uwezo kamishna jenerali kushikilia akaunti za benki za mtuhumiwa kwa muda, kwa mujibu wa kifungu kipya cha 50A kwa wauzaji wa dawa za kulevya za kiwandani.
“Pia, adhabu kwa makosa hayo itakuwa kifungo miaka 30 bila faini, ikumbukwe kuwa adhabu hii haiwahusu watumiaji wa dawa za kulevya ambao sheria inawachukulia kama wagonjwa endapo kutakuwa na uthibitisho wa daktari kwamba ni watumiaji na wameathirika na dawa hizo,” alisema Kakolaki.
Source: Muungwana
No comments:
Write comments