Katika kutekeleza juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda Shirika lisilo la kiserili la ACE - AFRICA limetoa msaada wa mashine ya kusagia na kukobolea nafaka kwa kikundi cha wajasiriamali cha Loluvo kijiji cha Oloitushula kata ya Musa kwa lengo la kufanya kiwanda cha usindikaji wa unga wa nafaka.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hiyo Meneja wa Idara ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ndugu Salumu Lubuva kwenye ofisi za kijiji cha Oloitushula amesema kuwa shirika la ACE AFRICA linaunga mkono juhudi za serikali kwa vitendo kwa kuwezesha wananchi kujiunua kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2035 kwa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Lubuva amesema kuwa shirika limetoa mashine kwa kikundi cha Loluvo yenye thamani ya shilingi 6,200,000/= kwa lengo la kuwawezesha wananchi hao kujikwamua kiuchumi na kubadilisha maisha yao, familia zao na jamii kwa ujumla.
Amefafanua kuwa mashine hiyo inatakiwa kufanyika kiwanda cha kusindika unga na kuweka kwenye vifungashio na kuuza kwa wingi zaidi kwenye masoko ya Musa na maeneo mengine.
Aidha Lubuva amefafanua kuwa kabla ya kuwakabidhi mashine wajasiriamali hao walianza kwa kuwapa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuweza kuendesha biashara ikiwa ni pamoja na kutunza kumbukumbu za mapato na matumizi, kutunza fedha, kuweka na kukopo, kutafuta masoko pamoja na kuziona fursa katika maeneo yao.
Hata hivyo Lubuva amewaasa wajasiriamali hao kusimamia vizuri mradi huo kwani endapo watashindwa kuendeleza mashine hiyo itanyang'anywa na kupeleka kwa wahitaji wengine na zaidi amewataka wajasiriamali hao kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za migogoro ya kuendesha biashara ya pamoja kwenye vikundi.
"Inapotokea kutokuelewana ni vema kukaa na kuzungumza kwa kushirikisha viongozi wa kata na kijiji pamoja na shirika letu ili kutatua mgogoro na kusonga mbele, tunatambua kunako mafanikio kuna changamoto nyingi hivyo jiandaeni kukabiliana nazo" amesema Lubuva
Naye mkuu wa kitengo cha uwezeshaji wananchi kiuchumi shirika la Ace Africa ndugu John Emanuel amesema kuwa wametoa mashine hiyo ili ifanyike kuwa kiwanda kidogo ambapo licha ya kutoa huduma ya kusaga na kukoboa nafaka za wananchi wanaowazunguka yawapasa kwenda mbele zaidi kwa kutengeneza unga kwa kufungasha kwenye mifuko na kuuza ndani na nje ya kata ya Musa.
"Mradi huu wa mashine muufanye kuwa kiwanda cha kusindika na kupark unga ili kuuza ndani na nje ya kata ya Musa hata mkoa mzima wa Arusha na Tanzania nzima sio kuishia kutoa huduma ya kusaga na kukoboa tuu" amesema John
Mwenyekiti wa kikundi cha Loluvo Bi. Upendo John ameonesha furaha yake ya kupata mashine hiyo bila kutoa fedha yoyote na kukiri kuwa mashine hiyo ni mkombozi wao na itawawezesha kujikwamua kiuchumi wao na jamii nzima ya wananchi wa Oloitusha.
Aidha amefafanua kuwa licha ya kuwa mashine hiyo inakwenda kuwapatia fedha za kuinua vipato lakini pia mashine hiyo itawezesha kusaidia jamii yao kupata huduma ya kusaga na kukoboa karibu zaidi tofauti na hapo awali ambapo huduma ya mashine haikuwepo kijijini hapo.
"Hiki ni kiwanda kidogo, mashine imekuja kutukomboa kwa kuwa tumekuwa tukipata huduma ya kusaga umbali wa zaidi ya kilomita kumi, tunaenda kusaga Nengun'gu kule Monduli au Kisongo madukani sasa huduma ipo nyumbani" amesema mwenyekiti huyo
Evaline Wlison mwanakikundi cha Loluvo methibitisha kuamini kuwa mashine hiyo itawakwamua kiuchumi na kuahidi kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kufikia malengo waliyoyakusudia wakati wa kuomba msaada huo wa mashine.
"Hii ni neema ya pekee kwetu,tunaahidi kwenda kuanza kazi mara moja na tutafunga mkanda kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojipangia wakati tunaomba mashine" amethibitisha Evaline
Aidha Shirika la Ace Africa linategeme kutoa mashine tatu ikiwa mashine mbili zimeshatotolewa moja kwa kikundi cha wajasiriamali wa kijiji cha Oloitushula na nyingine kijiji cha Ngorbob kata ya Matevesi na wanategemea pia kutoa mashine nyingine kwenye kijiji cha Olelosi kata ya Kimnyaki.
Shirika la Ace Africa linafanya shughuli mbalimbali za kijamii kwenye kata 12 za Tarafa ya Mukulat katika halmashauri ya Arusha ikiwa ni pamoja na uelimishaji wa Haki na ulinzi na usalama wa mtoto, Afya ya Lishe pamoja na uwezeshaji vikundu vya wananchi kiuchumi.
PICHA ZA MATUKIO YA MAKABIDHIANO YA MASHINE HIYO.
No comments:
Write comments