Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha Mh. Noah Lembris amewataka wananchi wa vitongoji vya Tarakwa na Saitabau kata ya Tarakwa kuachana na migogoro na malumbano baina yao kwa kuwa haina tija badala yake kukaa pamoja na kujipanga kuchangia maendeleo ya vitongoji na kata yao kwa ujumla.
Mwenyekiti Lembris ameyasema hayo wakati wa mkutano maalum uliofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya kata ya Tarakwa ulioitishwa na uongozi wa halmashauri ya Arusha baada ya kata hiyo kuwa na migogoro na kutokuelewana jambo lililosababisha mkwamo katika shughuli za maendeleo.
Mwenyeki huyo amewaeleza wananchi hao kuwa ni vema wakaachana na migogoro kwa kuwa haina tija kwao na kuongeza kuwa chuki, malumbano, kujiona bora kuliko mwingine ni tatizo katika maendeleo ya wananchi.
"Viongozi mnatakiwa kuweka pembeni tofauti zenu za kiitikadi kwa kuwa huu ni wakati wa kuwatumikia wananachi kwa dhamana waliyowapatia na si wakati wa malumbano"amesema Mwenyekiti huyo
Aidha Mheshimiwa Lembris amewataka viongozi kufanya kazi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu zinazoelekeza wazi majukumu ya kila kiongozi na kutambua majukumu ya mwingine pamoja na mipaka ya majuku ya kila mmoja na zaidi kila mmoja kuheshimu majukumu ya mwingine.
"Kanuni ziko wazi zinaelekeza nafasi ya kila mtu na umuhimu wake katika kuwatumikia wananchi si diwani, mwenyekiti, Afisa Mtendaji wa kata kila mmoja ana majukumu yake na mipaka yake ya kazi mkitambua na kuheshimu hayo hakutakuwa na malumbano" amesisitiza Mwenyekiti
Hata hivyo Mwenyekiti huyo amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha kusitisha kwa muda uhamisho wa Afisa Mtendaji wa kata hiyo na Afisa Mtendaji wa Kitongoji cha Saitabau mpaka hapo ukaguzi wa hesabu za kilichokuwa Chombo cha Watumia maji kukamilika.
Awali Chombo cha watumia maji kilichokua kikisimamia mradi wa maji wa Olasaita waligoma kukabidhi mradi huo wa maji kwa Mamlaka ya Maji Ngaramtoni NGAUWASA lakini sheria inaelekeza miradi yote ya maji kwenye eneo la Mamlaka ya mji mdogo Ngaramtoni kusimamiwa na NGAUWASA.
Hata hivyo licha ya mvutano na malumbano ya muda mrefu mkutano huo ulimalizika kwa maridhiano ya wananchi hao kuweka tofauti zao pembeni na kushikamana kwa maendeleo ya kata yao.
No comments:
Write comments