Dar es salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji kwa mtoto mdogo na kumwekea valvu mbili za moyo za bandia.
Teknolojia hiyo ambayo ni nadra kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, imefanyika chini ya jopo la madaktari kutoka Taasisi ya Moyo BLK ya India na JKCI, ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo.
Akizungumza baada ya upasuaji huo, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Peter Kisenge amesema kwa msaada wa wataalamu kutoka BLK wamefanikiwa kukamilisha upasuaji huo.
Amesema JKCI imekuwa ikifanya upasuaji wa kuweka valvu moja pekee, upasuaji ambao kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka jana.
"Upasuaji huu umewezekana kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki na Kati kwa msaada wa BLK. Mgonjwa huyu angepelekwa nje ingegharimu zaidi ya Sh35 milioni," amesema Dk Kisenge.
Amesema upasuaji huo umegharimu Sh14 milioni.
Mwenyekiti wa BLK ambaye ni daktari bingwa wa mishipa mikubwa ya damu, Dk Ajay Kaul amesema wapo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha inafanikiwa katika matibabu.
No comments:
Write comments