MKUU wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Jenerali Venance Mabeyo amezungumzia matukio ya uhalifu yanayoendelea nchini ya watu kupigwa risasi kuwa vyombo vya ulinzi vipo kazini na hivi karibuni hali itakuwa shwari.
Matukio makubwa ya watu kupigwa risasi yaliyotokea nchini hivi karibuni ikiwa ni pamoja na lile la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa TLS Tundu Lissu, aliyepigwa risasi Septemba 7 mjini Dodoma na watu wasiojulikana.
Aidha ameelezea tukio jingine la kupigwa risasi Jenerali mstaafu Vincent Mritaba aliyepigwa risasi na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi wakati akiingia nyumbani kwake eneo la Ununio wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam akitoka benki siku tatu zilizopita.
Mbunge Lissu kwa sasa yupo Nairobi nchini Kenya akiendelea na matibabu huku hali yake ikielezwa kubadilika badilika wakati Jenerali Mritaba anatibiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo ya Jijini Dar es Salaam na afya yake inaelezwa kuimarika.
HALI ITAKUWA SHWARI
Jenerali Mabeyo amesema hayo alipozungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana amesema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinashughulika na matukio kadiri yanavyojitokeza na anaamini hali itakuwa shwari.
“Matukio yanayoendelea tunakabiliana nayo, vyombo vya ulinzi na usalama wakati wote vinakabiliana na matukio kadiri yanavyojitokeza, Ninaamini hali itakuwa shwari na sasa vinashughulika.
“Hoja ya msingi tunataka kujiridhisha silaha hizi zinatoka wapi, hawa watu ni wa aina gani. Sasa vyombo mviachie vifanye kazi yake, msitoe majibu haraka, tukio linapotokea lazima uangalie limetokeaje, chanzo ni nini, na ‘motive’ (sababu) ni nini,” alisema Jenerali Mabeyo.
ASHANGAA MATUKIO YA SASA KUSHTUA WATU
Katika hatua nyingine, alionyesha kushangazwa na matukio ya sasa kuonyesha kushtua watu wengi, tofauti ya yaliyotokea Kibiti mkoani Pwani, yaliyoua zaidi ya watu 35.
“Kwa nini matukio yaliyotokea Kibiti hayaleti mshtuko mkubwa wakati watu walioathirika Kibiti ni wengi zaidi kuliko matukio ya sasa, mimi sitaki kuingia huko,” alisema.
WANAOTEKELEZA MATUKIO YA KUPIGA WATU RISASI
Alisema kwa matukio ya sasa ya kupiga watu kwa risasi, uzoefu unaonyesha wanaoyatekeleza ni watu ambao hawajapita kwenye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Vijana wanaohusika katika uhalifu hawajapitia Jeshi la Kujenga Taifa, kwa hiyo tuna imani kabisa vijana wetu wanaopitia Jeshi la Kujenga Taifa wanakuwa na maadili, wanakuwa na nidhamu, nitaomba ninyi mtusaidie katika wale watakaokuwa wamekamatwa katika kuwahoji, tuone kama watakuwa wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa,” alisema Jenerali Mabeyo.
SIRRO ATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO
Mbali na Jenerali Mabeyo, Mkuu wa Polisi, IGP Simon Sirro, alizungumzia suala la Lissu kupigwa risasi akiwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha kuwatia mbaroni wahalifu waliohusika.
“Naomba wananchi wasidanganywe kwenye suala zima la siasa na vitu vingine, huwa nasema siku zote, kama hakuna amani na usalama siasa haiwezi kupata nafasi, tukio hili limetokea, tunapeleleza na tupo makini na hili tukio.
“Kwa sasa tumeongeza vikosi vya upelelezi Dodoma, wale waliofanya lile tukio ni lazima tutawakamata, ila upelelezi huu unaweza kuzaa matunda mazuri zaidi endapo wananchi watatupa ushirikiano wa kutosha,” alisema IGP Sirro.
No comments:
Write comments