Tuesday, September 5, 2017

Mkataba Mlimani City kufumuliwa


Mkataba wa mradi wa Mlimani City ulio chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) unatarajiwa kufumuliwa baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwa una kasoro nyingi zikiwamo zenye harufu ya ufisadi.

Aidha, kutokana na utata huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ililazimika kumtimua Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Rwekaza Mukandala na watendaji wa chuo hicho, baada ya kufika mbele ya kamati hiyo jana bila Mwenyekiti wa Baraza la chuo chao ili kujibu hoja mbalimbali za CAG zikiwamo za suala hilo.

Katika mahojiano maalum na Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema kamati yake imeguswa na taarifa ya CAG kuhusiana na dalili za ‘upigaji’ wenye kuweza kudumu kwa miaka kati ya 50 na 85 kwa mujibu wa makubaliano, na hivyo watahakikisha mkataba huo unafumuliwa na kurekebishwa ili uwe na manufaa kwa pande zote mbili.

Alisema kamati yake, kabla ya kukutana na uongozi wa UDSM mjini hapa jana, iliomba kupewa mwongozo wa CAG jinsi mkataba huo unavyopaswa kurekebishwa kwa maslahi ya taifa.

"Mpaka wiki hii (iliyopita) inamalizika, tutakuwa tumeshapata taarifa kutoka kwa CAG ya jinsi gani mkataba utakuwa umerekebishwa ili uwe na manufaa kwa pande zote mbili.

WINGI WA DOSARI
Katika ripoti yake ya mwaka 2015/16 aliyoikabidhi kwa Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 27, mwaka huu, CAG Prof. Mussa Assad alianika udhaifu mkubwa katika mradi huo.

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma Aprili 13, mwaka huu, Prof. Assad alisema ujenzi wa mradi wa Mlimani City ulioanza Oktoba Mosi, 2004, ulikadiriwa kukamilika Septemba Mosi, 2016 au siku yoyote kabla ya tarehe hiyo, kwa makubaliano ya mkodishwaji na mkodishaji.

Hata hivyo, CAG alisema katika ukaguzi wake, amebaini mradi mdogo wa hoteli ya nyota tatu (inayopaswa kuwa na vyumba 100 kikiwamo chumba cha mikutano kinachochukua watu 1,000), na uboreshaji wa bustani ya botania, ikiwa ni sehemu ya mradi wa Mlimani City, haujakamilika kwa kipindi cha miaka 10 toka tarehe ya makubaliano ya kumaliza mradi.

"Ni mtazamo wangu kuwa hakuna ufuatiliaji wa karibu, usimamizi na tathmini ya mkataba huo kwa uongozi wa UDSM," Prof. Assad alisema katika taarifa yake ya ukaguzi wa hesabu za mashirika ya umma.

Aliongeza: "Kwa sababu hiyo, kuna uwezekano wa kushidwa kumalizia kazi iliyobaki kwa sababu ya ongezeko kubwa la gharama ya kumalizia mradi toka kipindi kilichopangwa kupita."

Anaishauri menejimenti ya UDSM kuuangalia upya mkataba iliongia na kampuni ya Mlimani City Holding kuharakisha umaliziaji wa miradi.

Prof. Assad pia anasema amebaini ukiukwaji wa ulipaji wa ada ya chuo kifungu cha 1.1(j) cha mkataba pamoja na kifungu 10.1 cha hati ya ukodishaji wa uwanja ambavyo vinaeleza kuwa UDSM inapaswa ipate asilimia 10 ya mapato ya kodi ghafi.

"Kinyume cha kifungu tajwa hapo juu, Mlimani Holding Limited (MHL) hufanya mahesabu ya gawio la kodi ya UDSM kwa kuzingatia asilimia 10 ya mapato ya kodi baada ya kutoa gharama za uendeshaji badala ya kujumuisha gharama za uendeshaji," Prof. Assad anasema.

Anabainisha kuwa ukiukwaji huo wa mkataba unaifanya UDSM kuwa katika hatari ya kupoteza kiasi kikubwa cha mapato kutoka katika mradi wa Mlimani City.

Prof. Assad anaishauri menejimenti ya chuo kupitia upya mahesabu ya gawio lake la asilimia 10 kutokana na mkataba na kuomba kulipwa na mpangaji kiasi kilichokuwa kimekosewa na pia kuwasiliana na mpangaji na kufikiria kubadilisha mkataba ili kuweka vifungu ambavyo vitaruhusu idara ya ukaguzi ndani ya chuo kuangalia mapato na gharama za uendeshaji wa mradi.

CAG pia anasema amebaini udhaifu katika ufuatiliaji na usimamizi wa mapato kutoka kwa wapangaji wadogo.

Alisema kifungu cha 11.2(l) cha hati ya makubaliano, kinamtaka mpangaji (MHL) kutopangisha mtu yeyote ambaye hajathibitishwa na mpangishaji (UDSM), lakini kinyume cha makubaliano hayo, Prof. Assad anasema amebaini MHL imepangisha majengo kwa wapangaji wengine bila kupata kibali cha chuo.

Prof. Assad alisema kuna upungufu wa utekelezaji wa vipengele vya mkataba kwa upande wa UDSM, hivyo kupelekea chuo hicho kushindwa kujua kwa usahihi mapato ya kodi kutoka kwa wapangaji wote.

Pia alisema amebaini kuna udhaifu mwingine wa kukosekana kwa haki ya UDSM kujua kazi zinazofanywa na MHL.

CAG alisema katika mapitio ya mkataba wa upangishaji wa ardhi kati ya UDSM na MHL, amegundua mkataba haumpi mmiliki wa ardhi (UDSM) haki ya kukagua kazi zinazofanywa na mpangaji (MHL).

"Katika hali hii, mpangishaji ambaye ni UDSM hawezi kujua endapo mpangaji (MHL) anakiuka mkataba katika uendeshaji au kuna baadhi ya wapangaji wa nyumba hawawekwi wazi na mpangaji huyu," alisema.

MGAWO WA MALI
CAG pia alisema katika mapitio ya mkataba huo, amegundua hauelezei hali halisi ya ugawanaji mali pindi mkataba utakapoisha (miaka 50 au 85) kutokana na makubaliano ya pande mbili.

Alisema hakuna makubaliano yoyote yanayoelezea mgawanyo wa mali na miondombinu itakayokuwapo wakati mkataba unaisha.

Alieleza kuwa katika hali hiyo, kuna uwezekano wa kutokea kwa mvutano wa kisheria mwisho wa mkataba na ikitokea, UDSM itakosa msaada wa kisheria.

Alishauri UDSM kuingia katika mazungumzo na MHL ili kuweka vifungu vitakavyoonyesha haki ya kila upande wakati mkataba utakapoisha.

KUTOLIPWA DOLA 58,000
CAG Assad pia alieleza kuwa ukaguzi wake umebaini USDM iliingia katika makubaliano na kampuni ya Ernst & Young kufanya ukaguzi maalum ili kujua kiasi cha mapato ambacho chuo kinaidai kampuni ya MHL katika kipindi cha kuanzia Mei Mosi, 2006 hadi Juni 30, 2014.

Alisema wakati wa ukaguzi, aligundua kuwa kiasi cha dola za Marekani 309,458 kilitakiwa kipokewe na chuo kutoka MHL, lakini usuluhisho wa mahesabu ulionyesha MHL ililipa dola za Marekani 213,850 kupitia uhamisho wa benki kwa njia ya kieletroniki na kubakisha dola za Marekani 57,607.

"Kuna ufuatiliaji duni kwa upande wa menejimenti ya UDSM katika kukusanya deni hilo. Menejimenti ya chuo inashauriwa kuongeza nguvu katika kufuatilia na kukusanya deni wanaloidai MHL," alisema.

PAC YAWATIMUA UDSM
Katika hatua nyingine, PAC jana iliwatimua watendaji wa UDSM akiwamo Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala, baada ya kufika mbele ya kamati hiyo bila Mwenyekiti wa Baraza la chuo kikuu hicho kikongwe zaidi nchini na chenye umaarufu barani Afrika.

Viongozi hao walifika kwenye kamati hiyo ili kuhojiwa kufuatia hoja za ukaguzi zilizotolewa na CAG za mwaka 2015/16.

Kabla ya kuanza kwa mahojiano hayo, Mwenyekiti wa PAC, Kaboyoka alihoji sababu za Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Peter Ngumbulu kutohudhuria.

Katika majibu yake, Prof. Mukandala alisema kuwa katika barua ya kuutaarifu uongozi wa chuo hicho kufika mbele ya kamati hiyo, ilielekeza Ofisa Masuhuri aambatane na Mhasibu Mkuu, Ofisa Ugavi na wakuu wa idara ambao Ofisa Masuhuri anaona watasaidia katika kujibu hoja kwenye kamati.

"Kwa hiyo, naomba msamaha wako Mheshimiwa Mwenyekiti, labda sikuelewa vizuri lakini mimi nilifuata maelekezo ambayo tulikuwa tumepewa," alisema Prof. Mukandala.

Baada ya majibu hayo, Kaboyoka alihoji Ofisa Masuhuri ni nani kati ya maofisa wa UDSM waliokuwa wamefika mbele ya kamati yake jana na Prof. Mukandala alijibu kuwa anachofahamu yeye mwenyewe ndiyo Ofisa Masuhuri (Makamu Mkuu wa Chuo).

Kutokana na majibu hayo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hillary, alisema ni lazima mwenyekiti wa baraza hilo afike mbele ya kamati hiyo na kwamba kwa taarifa ambayo huwa wanapewa huwa wanatakiwa kuhudhuria wakiwa naye.

"Barua iliyoandikwa na Msajili wa Hazina inaweza ikawa ilichelewa kufika," Aeshi alisema, "kwa kawaida inatakiwa mwenyekiti wa baraza ahudhurie kwenye kamati."

Mjumbe wa kamati hiyo na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM), alionekana kushtushwa na kuwapo kwa maofisa wengi waliofika mbele ya kamati hiyo wakiwakilisha wakuu wa idara husika.

"Katika utambulisho wa watendaji wa chuo, nimeona kuna makaimu wengi, ni vyema watakapofika tena kwenye kamati waje wakuu wa vitengo husika," alisema.

Kutokana na hali hiyo, Kaboyoka aliamua kuwarudisha watendaji hao na kuwataka kufika mbele ya kamati hiyo kesho wakiwa na Mwenyekiti wa Baraza la chuo.

Alisema hesabu za chuo hicho hazipo vizuri, hivyo wanahitajika wahusika wenye uwezo wa kujibu hoja za wajumbe wa kamati yake na si watendaji wanaokaimu.

"Chuo tunachokitegemea kama Chuo Kikuu (cha Dar es Salaam), kinachofundisha watu mbalimbali halafu kinakwenda kinyume inashangaza," alisema Kaboyoka.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo