Wednesday, September 20, 2017

Mama aliyebomolewa nyumba Olturoto kutokana na mafuriko apewa msaada wa vifaa vya ujenzi


Halmashauri ya Arusha kupitia fedha za mapato ya ndani imetoa msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ta shilingi 750,000 kwa mama aliyebomolewa nyumba na mafuriko yaliyotokana na mvua zilizonyesha mwaka 2014 na kumuacha hana mahali pa kuishi na watoto kwa muda mrefu.

Hatimaye kilio cha muda mrefu cha mama huyo anayejulikana kwa jina la Domina Bartazari mkazi wa kata ya Olturoto kinaelekea kufika mwisho baada ya kukabidhiwa jumla ya bati 15 na mifuko 50 ya saruji kwenye ofisi za makao makuu halmashauri ya Arusha.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha, Afisa Mipango wa Halmashauri Annastazia Tutuba amesema kuwa Halmashauri imefikia kutoa msaada kwa mama huyo kutokana na adha kubwa aliyokuwa akiipata yeye pamoja na watoto kutokana na kukosa mahali pa kuishi kwa muda mrefu.

Tutuba amefafanua kuwa licha ya changamoto nyingi ambazo zinawakabili wananchi wengi ndani ya halmashauri lakini mama huyu alikuwa na shida kubwa ya mahali pa kuishi na watoto na kuongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya majukumu ya halmashauri kuisaidia jamii yenye mahitaji ya lazima pale inapobidi.

Aidha Afisa Mipango huyo amemtaka mama huyo kuhakikisha kuwa ametumia vifaa  hivyo alivyokabidhiwa kwa kujenga nyumba kama alivyoomba na si vinginevyo jambo ambalo litamuondolea adha ya mahali pa kuishi na watoto.

" Kupewa vifaa ni hatua ya kwanza lakini hatua inayofuata ni kutumia vifaa hivi kwenye ujenzi wa nyumba kama ulivyoomba na zaidi tunakutakia kila la kheri katika kukamilisha ujenzi huo" amesisitiza Tutuba

Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo Bi.Domina Bartazari ameshukuru uongozi wa Halmashauri kwa msaada wa vifaa hivyo na kuahidi kwamba atavitumia vifaa hivyo kwa kujenga nyumba kama alivyoomba.

"Nyumba yangu ilibomolewa na mafuriko tangu mwaka 2014 nimehangaika sana kutafuta msaada hatimaye leo serikali imeniona na kunisaidia sina la kusema zaidi ya kushukuru" amesema Domina

Hata hivyo Domina hakusita kuonysha hisia zake kwa kumshukuru kwa  dhati Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha Dk. Wilson Mahera kwa kumsikiliza na kuona tatizo alilokuwa nalo na kuweza kumpatia msaada huo utakaomuwezesha kupata nyumba ya kuishi yeye pamoja na watoto wake.






No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo