Monday, September 18, 2017

Arusha: Polisi yatoa ufafanuzi watoto waliokufa kwa kulipukiwa na bomu.


Kamanda wa polisi wa  mkoa  wa Arusha  Bw.Charles Mkumbo amewataka viongozi katika maeneo yaliyoko karibu  na  kambi  za  mazoezi ya kijeshi kuweka  utaratibu wa kuwakumbusha wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona vitu  wasivyovijua hasa vyenye asili ya chuma ili kuepusha madhara yasiyo ya  lazima.

Kamanda Mkumbo ametoa hadhari hiyo alipokuwa akizungumzia tukio la vifo vya  watoto  watatu wakazi wa kata ya Lokisale wilayani  Monduli vilivyosababishwa  na mlipuko wa bomu  waliookota wakati   wanachunga  mifugo na kuanza  kulichezea kama mpira ambalo lililipuka na kuwajeruhi vibaya miguuni.

Akizungumza kwa njia ya simu kamanda Mkumbo amesema licha ya kuwa tukio hilo ni la  bahati mbaya lakini lingeweza kuepukika kama  watoto hao wangeweza  kuepuka  na kutoa taarifa ya kitu walichokiona suala ambalo pia wangeweza  kufanya  hivyo  kama  wangekuwa  wanakumbushwa  na  wazazi  wao mara kwa  mara  wanapokwenda  machungani.

Akizungumza pia kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya Monduli Bw. Iddy Kimanta  amesema watoto hao wote ni wanafunzi  wa shule ya msingi Nafuko na wawili   akiwemo Landisi  Setabau miaka 12 na Samweli Nyandusi miaka  9  walikuwa  wanasoma darasa la kwanza  wakati  mwingine aliyetajwa kwa jina la Seuri  Losila miaka 9 alikuwa darasa la tatu.

Viongozi wa eneo lililopotokea tukio hilo wamesema kimsingi tukio hilo ni  bahati mbaya kwani kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakielimishwa na wanaelewa  na  pia kufuata maelekezo na mara nyingi wamekuwa wakishitoa  ushirikiano  ukiwemo wa kutoa taarifa wanapoona mabaki ya vyuma na kwamba kimsingi ni tukio  la bahati mbaya.

Kwa mujibu wa viongozi hao katika maeneo mengi ya wafugaji wakati wa likizo  watoto huwasaidia wazazi wao   kuchunga  mifugo na  pia  wakati wote   wamekuwa wakitoa taarifa wanapokutana na vitu kama hivyo na wahusika  wamekuwa  wakifika  mara  moja na kuvichukua  

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo