Friday, August 4, 2017

Wamiliki mashamba makubwa kitanzini

Serikali inaendelea na jihada za kuwadhibiti wafanyabiashara wa mashamba makubwa wanaoyatumia kwa ajili ya kukopea fedha kwenye taasisi za fedha na kisha kutoyaendeleza.

 Zoezi hilo linatarajiwa kuanza rasmi mapema ujao wa 2018 na kuwasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ardhi, utakaowadhibiti wafanyabiashara hao.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kubaini uwepo wa mashamba mengi yakiwemo yanayomilikiwa na wafanyabiashara wakubwa nchini ambayo hayajaendelezwa huku yakiwa yamekopewa fedha nyingi na kutumika katika biashara nyingine na kuyatelekeza mashamba hayo yakiwa mapori.

Akizungumza na magazeti ya Serikali ya HabariLeo na Daily News ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusiluka alisema sheria hiyo italenga kudhibiti watu kutumia mashamba kujipatia fedha na kisha kuyatelekeza.

“Tunataka kupitia sheria hii, mtu akikopa kupitia mashamba haya, fedha hizo zitumike kuyaendeleza na siyo kuyaacha mapori na kufanya biashara zake nyingine. Sheria itaweka masharti kuwa mikopo yote yenye dhamana ya mashamba, isimamiwe na benki zenyewe,” alisema.

Ameeleza kuwa katika mpango unaoendelea kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya kufanya ukaguzi wa mashamba yasiyoendelezwa wamebaini mashamba mengi ambayo hayajaendelezwa na baadhi ya mashamba hayo yamechukuliwa mikopo benki. 

“Mashamba yote yasiyoendelezwa baada ya kufuata taratibu zote, ikiwemo kutoa notisi kwa wamiliki tumeyawasilisha kwa Rais John Magufuli kwa ajili ya kubadilishiwa umiliki, sheria inaturuhusu kuyataifisha pia kuyataifisha mashamba yaliyochukuliwa mkopo,” amefafanua Dk. Kusiluka

 Hata hivyo, alisema tunafanya mazungumzo na benki husika kuhusu mashamba hayo yaliyochukulia mikopo kwa sasa ili kuangalia namna ya wahusika wa mashamba hayo kubadili dhamana za mikopo yao ili yaweze kurejeshwa mikononi mwa serikali.

“Tunafanya hivi si kwa sababu hatuna uwezo wa kuyachukua la hasha, tunafanya hivi ili kunusuru benki hizi, kwani mashamba mengi yamechukulia mikopo mikubwa endapo tutayataifisha na kuyachukua kama hakuna dhamana nyingine" amesema

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo