Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kutumia mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama 'Government Electronic Payment Gateway' (GePG) katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na tozo nyingine zinazotokana na sekta ya Ardhi.
Mfumo huo utamrahisishia mwananchi kulipa kodi ya pango ya Ardhi popote alipo, ikiwa ni pamoja na kulipia tozo nyingine mbalimbali za sekta ya ardhi na pia mfumo wa GePG.
Mfumo huo pia utamuwezesha mwananchi anayemiliki kipande cha ardhi kujua anadaiwa kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi na kulipia popote alipo bila kusumbuka kufuata huduma hizo katika vituo vya makusanyo.
Kupitia mfumo huo mwananchi yeyote anayemiliki kiwanja au shamba lililopimwa na kuwa na hati, ataweza kutumia simu yake ya mkononi kujua kiasi cha kodi ya pango la ardhi anachodaiwa na kulipa kwa kutumia simu yake ya mkononi pia.
Majaribio ya ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki yalifanywa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, na kuonyesha mafanikio makubwa.
Kwa sasa elimu imetolewa kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es salaam kabla ya zoezi hilo kuhamishiwa Mikoa mingine hapa nchini.
No comments:
Write comments