Sunday, July 9, 2017

Waliokata rufaa ya vyeti feki waelekezwa pakwenda



WIZARA ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imewataka watumishi waliotajwa katika sakata la vyeti feki vya kidato cha nne, sita na ualimu, kuwasiliana na waajiri wao ili wapewe matokeo ya hatima ya rufaa zao.

Kauli hiyo imetolewa baada ya kuwapo kwa orodha ya majina ya uongo yanayosambaa katika mitandao ya kijamii, yanayodaiwa kutolewa na wizara hiyo, kwamba ni rufaa za wenye vyeti feki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Florence Temba, watumishi hao waliowasilisha rufaa za vyeti vyao katika Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), wanapaswa kufuatilia uhalali wa vyeti hivyo kwa waajiri na si katika mitandao.

“Ipo taarifa inayosambaa katika mitandao  mbalimbali, ikiwa na majina ya wanaodaiwa kuwa ni watumishi wa umma na maeneo yao, na kinachodaiwa ni matokeo ya rufaa zilizokatwa kuhusu uhalali wa vyeti vya elimu kwa wahusika,” ilisema taarifa ya wizara.

Pia ilisema taarifa inayosambaa mitandaoni haijatolewa na Serikali na ipuuzwe.

Kwamba watumishi wa umma na wananchi wote wanaelekezwa kuwa Serikali ina utaratibu rasmi wa kutoa taarifa na mawasiliano.

Aprili 28, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alimkabidhi Rais Dk. John Magufuli majina 9,932 ya watumishi wanaodaiwa kuwa na vyeti feki.

Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Magufuli, aliagiza watumishi hao kuondoka wenyewe kazini hadi ifikapo Mei 15, mwaka huu na wasipofanya hivyo watafikishwa mahakamani.

Pia Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Laurean Ndumbaro, aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema idadi ya watumishi waliokata rufaa Necta ni ndogo.

Alisisitiza kuwa watumishi wengi waliokata rufaa ni wale waliobadili majina baada ya  kaolewa na kuanza kutumia la mume, lakini hakuwasilisha vyeti vya ndoa.

Alisema kundi hilo na wengine kwa wakati huo walifanikiwa kuhakiki na kuendelea  na kazi, lakini wengi waliohakikiwa walikuwa na vyeti feki.

Ndumbaro alisema uhakiki wa rufaa hizo umesababisha kukwamisha kutolewa kwa awamu ya pili ya watumishi wenye vyeti feki kwa taasisi na wizara zake zilizobaki.


source;Muungwana Blog

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo